BAADHI YA ALAMA ZA KIYAMA ALIZO ZITAJA MTUME AMBAZO ZIMESHA TOKEA

Sifa njema zote ni haki ya Allah; Mola wa viumbe wote. Yeye pekee ndiye wa kuabudiwa na kuombwa. Rehema na Amani zishuke juu ya Bwana wetu Muhammad bin Abdillah, maswahaba wake na kila aliye itika mwito wake na kufuata maagizo yake mpaka siku ya Kiyama.
Baada ya kujifunza kuhusiana na siku ya Kiyama na vipengele vyake katika darasa zilizo pita, leo kwa msaada wake Mola tutaanza kuangalia baadhi ya Alama za Kiyama kama zilivyo tajwa na Mtume wa Allah, ambazo tayari zimesha tokea, tunaishi nazo katika maisha yetu ya kila siku. Tutazieleza alama hizo ili sisi na nyinyi tupate kuchukua mazingatio na kutambua kuwa Kiyama ki karibu mno.
Ndugu msomaji wetu-Allah akurehemu-ni vema ukajua ya kwamba kabla ya kuja kwa Kiyama, kuna Alama kadhaa andamizi zilizo tajwa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ambazo nyingi miongoni mwake zimesha tokea na nyingine bado hazijashuhudiwa. Zile ambazo zimesha tokea, zimepewa jina la “Alama ndogo za Kiyama”, na zile ambazo hazijatokea na zitatokea karibu kabisa na Kiyama, hizo zinaitwa “Alama kubwa za Kiyama”. Huu ndio ukweli tunao paswa kuufahamu kuhusiana na Kiyama na Alama zake kama unavyo elezwa na Qur-ani Tukufu:
ﻓَﻬَﻞۡ ﻳَﻨﻈُﺮُﻭﻥَ ﺇِﻟَّﺎ ﭐﻟﺴَّﺎﻋَﺔَ ﺃَﻥ ﺗَﺄۡﺗِﻴَﻬُﻢ ﺑَﻐۡﺘَﺔٗۖ ﻓَﻘَﺪۡ ﺟَﺎٓﺀَ ﺃَﺷۡﺮَﺍﻃُﻬَﺎۚ ﻓَﺄَﻧَّﻰٰ ﻟَﻬُﻢۡ ﺇِﺫَﺍ ﺟَﺎٓﺀَﺗۡﻬُﻢۡ ﺫِﻛۡﺮَﻯٰﻬُﻢۡ ١٨
“ Kwani wanangojea jengine isipo kuwa iwafikie Saa (ya Kiyama) kwa ghafla? Na hakika alama zake zimekwisha kuja. Na itapo wajia kutawafaa wapi kukumbuka hapo”. Muhammad [47]:18
Ndugu msomaji wetu mwema-Allah akurehemu-ni vema ukatambua mapema kabisa ya kwamba, hatukuletei mfululizo huu wa Alama za Kiyama uzisome tu pakesha, laa hasha. Bali lengo na madhumuni ni kuwaidhika, kuchukua mazingatio na mwisho ni kufanya maandalizi ya hicho Kiyama leo kabla ya kesho. Tusome pamoja:
ﺇِﻥَّ ﻓِﻲ ﺫَٰﻟِﻚَ ﻟَﺬِﻛۡﺮَﻯٰ ﻟِﻤَﻦ ﻛَﺎﻥَ ﻟَﻪُۥ ﻗَﻠۡﺐٌ ﺃَﻭۡ ﺃَﻟۡﻘَﻰ ﭐﻟﺴَّﻤۡﻊَ ﻭَﻫُﻮَ ﺷَﻬِﻴﺪٞ ٣٧
“ Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia”.
Qaaf [50]:37
Sasa basi tufuatane pamoja kuzisoma, kuzijua, kuzifahamu na kisha kuzifanyia kazi, miongoni mwa Alama ndogo za Kiyama zilizo elezwa na Mtume wa Allah ni pamoja na:
I. Kudhihiri kwa Wapiga watu kwa uonevu na dhulma pasina huruma na Wanawake watembea uchi.
Ndugu msomaji wetu-tambua na ufahamu ya kwamba watu kupigwa kwa uonevu na dhulma na wanawake kutembea uchi majiani, hizo ni miongoni mwa alama za Kiyama zilizo kwisha elezwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Tumtegee sikio la umakini na usikivu Mtume wetu akitueleza kuhusu hayo, anasema:
ﻧﺺ ﺍﻟﺤﺪﻳﺚ ﺑﺎﻟﻌﺮﺑﻴﺔ
Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwamba yeye amesema: “Mbeya (aina) mbili za watu wa motoni bado sijaziona; watu wenye mijeledi kama mikia ya ng’ombe wanayo wapigia watu. Na wanawake walio vaa lakini wako uchi, watembeao kwa madaha, wenye kupondoa (nyoyo za wanaume), vichwa vyao ni kama nundu ya ngamia yenye kuelemea upande. (Hao) hawataingia peponi na wala hawatainusa harufu yake na hakika harufu yake inanuswa toka umbali wa mwendo kiasi kadha na kadha”.
Na katika upokezi mwingine: “Na hakika harufu yake inanuswa kutokea umbali wa mwendo wa miaka mia tano”. Muslim-Allah amrehemu.
Hadithi hii ni mojawapo ya miujiza ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwa kuyaeleza kwake mambo ambayo hayakuwepo katika zama zake, ambayo yanatokea leo katika zama zetu kama alivyo yaeleza. Huyo ndiye Mtume wa Allah aliye itwa hata na maadui zake
“Mkweli Muaminifu”, ameishi katika zama zetu kabla ya kuishi kwetu katika zama zetu wenyewe. Zama ulio kithiri humo ufisadi kwa aina zake zote, zama zilizo sheheni mmomonyoko wa maadili kwa kiwango cha kukaribia kubomoka, zama ambazo kumeenea humo kutembea uchi baina ya wanawake. Kutembea uchi kuliko pambwa kwa majina mazuri “Ustaarabu”, “Maendeleo”, “Uhuru wa binaadamu”, “Mashindano ya ulembo” na baki ya majina mengineyo. Zama ambazo mtembea na mkaa uchi hutuzwa, zama ambazo mwanaadamu kumuonea na kumdhulumu mwenzake ni jambo la kupongezwa. Zama zilizo kosa utu seuze dini! Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuelezea kuhusiana na watu wa motoni khususan mbeya mbili miongoni mwao. Akawataja:
1. Madhaalimu ambao wanawaonea na kuwadhulumu waja wa Allah pasina haki kwa kuwapa vitisho au kipigo kikali, kuwadhalilisha, kuwaadhibu na kuwatesa kinyama kabisa. Wanayatenda hayo kwa ajili tu ya kutaka kuonyesha wao ni kina nani au kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kisiasa au kwa ajili ya kupata utajiri wa Dunia hii. Kwao kumwaga damu za wenzao ni sawa na kumchinja kuku wa kitoweo.
Bwana Mtume ameleta taswira ya madhaalimu hao kama kwamba anawaona na kuwashuhudia wakitenda unyama wao huo. Amewasawirisha wakiwa na mijeledi migumu inayo shabihiana na mikia ya ng’ombe iliyo kauka, wakiwashushia watu visago na vipigo vikali visivyo na chembe ya huruma, visivyo sikia kilio na machungu ya wadhulumiwa. Watu hao hawamuhurumii yeyote kwa udhaifu wake (kilema/mgonjwa/mwanamke/kikongwe) na wala hawamuheshimu mtu kwa cheo au utu uzima wake, wao wanacho jua ni kuadhibu tu.
Haya aliyo yaeleza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-sisi sote ni mashahidi, tunayashuhudia na kuyaona yakitendeka na kutokea miongoni mwetu ulimwenguni kote. Tunayaona yakitendwa na wapambe wa watu wenye pesa na wenye madaraka, watu wasio muogopa Allah, wasio jali kile kisimamo kitishacho, Allah anawaambia:
ﺃَﻟَﺎ ﻳَﻈُﻦُّ ﺃُﻭْﻟَٰٓﺌِﻚَ ﺃَﻧَّﻬُﻢ ﻣَّﺒۡﻌُﻮﺛُﻮﻥَ ٤ ﻟِﻴَﻮۡﻡٍ ﻋَﻈِﻴﻢٖ ٥ ﻳَﻮۡﻡَ ﻳَﻘُﻮﻡُ ﭐﻟﻨَّﺎﺱُ ﻟِﺮَﺏِّ ﭐﻟۡﻌَٰﻠَﻤِﻴﻦَ ٦
“ Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa. Katika siku iliyo kuu. Siku watakapo msimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote?”. Al-Mutwafifiina [83]:04-06
Wanaadamu hawa walio tajwa na Mtume wa Allah kuwa ni miongoni mwa watu wa motoni, wasio hata na chembe ya huruma mioyoni mwao, wamekuwa wabaya mno kuliko hata wanyama wa mwitu. Wanawasulubu, wanawatesa na kuwaadhibu wenziwao kama kwamba wao wataishi milele katika ulimwengu huu, hawatakufa na kwenda kuhukumiwa mbele ya Mola wao kwa matendo yao hayo maovu. Uovu wao huo ujulikanao na kuonekana na kila mmoja wetu, ni alama miongoni mwa alama ambazo ni kielelezo cha kukaribia mno kwa Kiyama. Tafakari na anza kuchukua hatua sasa kwa kutenda amali njema zitakazo kuwa watetezi wako katika siku hiyo nzito inayo tujongelea kwa kasi mno.
Haya sasa tulihitimishe somo letu hili la leo kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe Mola wetu Mkarimu. Tuombe:
ﺭَﺑَّﻨَﺎ ﭐﻏۡﻔِﺮۡ ﻟِﻲ ﻭَﻟِﻮَٰﻟِﺪَﻱَّ ﻭَﻟِﻠۡﻤُﺆۡﻣِﻨِﻴﻦَ ﻳَﻮۡﻡَ ﻳَﻘُﻮﻡُ ﭐﻟۡﺤِﺴَﺎﺏُ ٤١
“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41
ﺭَّﺑَّﻨَﺎٓ ﺇِﻧَّﻨَﺎ ﺳَﻤِﻌۡﻨَﺎ ﻣُﻨَﺎﺩِﻳٗﺎ ﻳُﻨَﺎﺩِﻱ ﻟِﻠۡﺈِﻳﻤَٰﻦِ ﺃَﻥۡ ﺀَﺍﻣِﻨُﻮﺍْ ﺑِﺮَﺑِّﻜُﻢۡ ﻓََٔﺎﻣَﻨَّﺎۚ ﺭَﺑَّﻨَﺎ ﻓَﭑﻏۡﻔِﺮۡ ﻟَﻨَﺎ ﺫُﻧُﻮﺑَﻨَﺎ ﻭَﻛَﻔِّﺮۡ ﻋَﻨَّﺎ ﺳَﻴَِّٔﺎﺗِﻨَﺎ ﻭَﺗَﻮَﻓَّﻨَﺎ ﻣَﻊَ ﭐﻟۡﺄَﺑۡﺮَﺍﺭِ ١٩٣ ﺭَﺑَّﻨَﺎ ﻭَﺀَﺍﺗِﻨَﺎ ﻣَﺎ ﻭَﻋَﺪﺗَّﻨَﺎ ﻋَﻠَﻰٰ ﺭُﺳُﻠِﻚَ ﻭَﻟَﺎ ﺗُﺨۡﺰِﻧَﺎ ﻳَﻮۡﻡَ ﭐﻟۡﻘِﻴَٰﻤَﺔِۖ ﺇِﻧَّﻚَ ﻟَﺎ ﺗُﺨۡﻠِﻒُ ﭐﻟۡﻤِﻴﻌَﺎﺩَ ١٩٤
“ Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumemsikia mwenye kuita akiitia Imani kwamba muaminini Mola wenu Mlezi, nasi tukaamini. Basi tusamehe madhambi yetu, na utufutie makosa yetu, na utufishe pamoja na watu wema. Mola wetu Mlezi! Na utupe uliyo tuahidi kwa Mitume wako, wala usituhizi siku ya Kiyama. Hakika Wewe huvunji miadi”. Aali Imraan [03]:193-194
Aamina!
Mpaka hapa tunataraji kwa msaada wake Mola utakuwa umesha anza kupata taswira ya Alama za Kiyama tunazo ziona kila kukicha na tunazo ishi nazo mitaani kwetu, kazini kwetu na shuleni kwetu. Alama zilizo tajwa na Mtume wa Allah. Juma lijalo kwa uweza wake Mola tutaendelea kuzungumzia kwa ufafanuzi mbeya ya pili ya watu wa motoni iliyo tajwa katika Hadithi.
Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Maoni