Jeshi la Somalia lasema Raia 10 waliuawa kwa makosa Bariire

Ndugu wa waliouawa kwa makosa nchini Somalia wakichukua maiti.

Jeshi la Somalia limesema kuwa vikosi vyake vikisaidiwa na vikosi vya Jeshi la Marekani vimewapiga risasi Wasomali 10 wakiwemo watoto watatu wakati wa operesheni iliyofanyika karibu na mji wa Bariire mapema Ijumaa asubuhi.

Jenerali Ahmed Jimale Irfid, mkuu wa majeshi ya Somalia aliyezungumza na VOA kutoka Mogadishu amethibitisha kuwa watu hao 10 ni raia wakiwemo watoto na wazee na kuwa waliuawa kwa makosa wakati wa operesheni hiyo katika shamba hilo lilioko katika mji wa Bariire, kilomita kama 55 kusini magharibi ya Mogadishu.

Hicho kilikuwa sio kitendo cha makusudi. Ni ajali na kukosekana kuelewana kwa pande mbili hizo; yaani vikosi vya jeshi na wakulima wa eneo hilo.

“Ilikuwa asubuhi mapema Ijumaa wakati bado kukiwa giza, na vikosi vikadhani kuwa wakulima hao ni wanachama wa al-Shabaab; baadhi ya wakulima walikuwa na silaha; kulikuwa na kutupiana risasi, hatujui ni upande gani ulianza kufanya hivyo na hivi ndio tukio lilivyokuwa,” Irfid amesema.

“Naweza kuthibitisha kuwa wale waliouawa katika tukio hilo wote walikuwa raia na wakulima; si kweli kwamba walikuwa ni wanachama wa al-Shabaab kama ilivyokuwa imeelezwa awali na viongozi wa serikali. Miili ya marehemu hao imeletwa katika Hospitali ya Mogadishu na mtu yoyote anaweza kwenda kuiona miili hiyo ikiwa ni lazima,” Jenerali amesema.

Jenerali amesema kuwa vikosi vya Marekani vilikuwepo katika tukio hilo, lakini hawezi kusema iwapo walikuwa ni sehemu ya vikosi vilivyohusika katika kuwauwa raia hao.

Kituo cha Africa command cha Marekani katika tamko lake kimesema “wanataarifa juu ya madai ya kuuawa raia karibu na mji wa Bariire, Somalia. Tunachukua maadai yoyote ya vifo vya raia wasio na hatia kwa umuhimu mkubwa na kwa kufuata viwango, tunatathmini juu ya tukio hilo ili kuweza kupata ukweli ulivyo kutoka katika eneo la tukio.”

Jenerali huyo amesema kuwa wameshakubaliana kukutana na maafisa wa jeshi la Marekani Jumamosi kulizungumzia suala hili.

Jenerali Irfid amesema amekutana na rais na waziri mkuu Ijumaa na wote wawili wameshtushwa na kusikitishwa na vifo vya raia hao.

Rais na waziri mkuu wamepeleka rambirambi zao kuhusiana na vifo vya raia hao.

“Serikali kwa upande wake mara moja imeunda kamati ya kutafuta ukweli juu ya tukio hilo na kujua sababu iliopelekea raia hao kuuawa,” Jenerali amesema.

Maoni