Kimwaga kufanyiwa upasuaji Afrika Kusini


WINGA wa kushoto wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Joseph Kimwaga, anatarajiwa kuondoka nchini muda wowote kuanzia sasa kuelekea Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji wa goti lake la mguu wa kushoto.

Kimwaga aliteguka goti lake hilo Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu cha TTC cha mkoani Mtwara, wakati Azam FC ikijiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ndanda ulioisha kwa mabingwa hao kushinda bao 1-0 wikiendi iliyopita.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabuwww.azamfc.co.tz Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, alisema kuwa awali mchezaji huyo ilibidi afanyiwe kipimo cha MRI lakini ilishindikana kutokana na Kimwaga kuwahi kuwekewa kipande cha madini (metal) huku nyuma alipokuwa amekatika ‘ligament’ ya kati kwenye goti lake hilo.

“Kwa hiyo kipimo cha MRI hakikuweza kufanyika, kilichofanyika ni ‘Ultra Sound’, ambayo ilithibitisha kwamba ndani ya goti lake kuna maji mengi na damu nyingi,” alisema.

Mwankemwa alisema matibabu yake yapo ya aina mbili, ya kwanza ni kumfanyia upasuaji wa goti ili kuweza kujua tatizo ni nini na kuweza kutibu, ambapo kwa matibabu hayo itamfanya Kimwaga kurejea uwanjani baada ya miezi tisa.

“Matibabu kwa njia ya pili ni kumfanyia ‘Arthroscopic’, ambacho ni kipimo maalum kinachofanya mambo mawili kinaweza kugundua tatizo na vilevile kikafanya matibabu, mapendekezo ni kwamba ilikuwa ni lazima akafanyiwe kipimo hiki kwani itamchukua miezi miwili tu kurejea dimbani,” alisema.

Maoni