Kura zinaendelea kuhesabiwa na matokeo kutangazwa baada ya

Kura zinaendelea kuhesabiwa na matokeo kutangazwa baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya Jumanne.
Katika matokeo yaliyokuwa yametangazwa kufikia saa kumi alfajiri, Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee alikuwa akiongoza akiwa na kura 6,574,087 (55.21%) akifuatwa na Raila Odinga wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) aliyekuwa na kura 5,236,724 (43.98%) Matokeo hayo ni ya vituo 31947 kati ya 40,883.
Kura ambazo zilikuwa zimeharibika kufikia wakati huo ni 307,252.
Katika baadhi ya vituo, shughuli ya upigaji kura ilichelewa kuanza na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) iliongeza muda kufikia wakati uliokuwa umepotezwa kabla ya kufungua vituo.
Kisheria, vituo vilitakiwa kufunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni saa za Afrika Mashariki.
Lakini katika baadhi ya maeneo, mvua kubwa ilitatiza uchukuzi na upigaji kura na kwingine hitilafu za kimitambo zikachangia kukwamisha upigaji kura. Muda wa kufungwa kwa vituo uliongezwa kwa vituo vilivyochelewa kufunguliwa.

Maoni