Madee awachana wa 'kimataifa'.

Msanii Madee amewafunguka juu ya wasanii wanaolazimisha kufanya vitu vikubwa vilivyo nje ya uwezo wao, ili muziki wao kwenda kimataifa kama ambavyo wengi wanakusudia, na kusema kuwa haitakiwi kuwa hivyo.
Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio alipokuwa akitambulisha kazi yake mpya 'Sikila' ambayo amemshirikisha msanii wa Nigeria Tekno, Madee amesema kazi kwenda kimataifa zinakuja zenyewe baada ya kufanya kazi nzuri, akitolea mfano ufanyaji wa kazi zake.
"Mimi siyo yule mtu ambaye nafanya kitu kwa sababu nataka kwenda kimataifa, unapoamua kufanya kitu unafanya, kwa sababu kimataifa haiji kwa sababu wewe unataka, kimataifa inakuja yenyewe kila unachokifanya kinasogea tu, ukijifanya kulazimisha mwisho wa siku ndiyo unakuwa unaangukia pua, unaenda kufanya mavideo ya gharama huko unatoa hela unampa nani, mwisho wa siku hamna kitu unapata mawazo, mimi nafanya muziki ambao nauona ni tofauti", alisema Madee.
Madee aliendelea kusema kuwa ukifanya kitu chenye ubora na chenye kuleta utofauti, huwa kinajiuza chenyewe na kufika huko kunakoitwa kimataifa.

Maoni