MATCH REPORT: KCCA 1-1 Azam FC

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya KCCA katika mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu ujao uliofanyika Uwanja wa StarTimes, jijini Kampala, Uganda.
Mchezo huo uliokuwa mkali na wa aina yake ulishuhudia ukimaliza kipindi cha kwanza kwa timu zote zikiwa hazijafungana, na kipindi cha pili kila upande ukafanikiwa kucheka na nyavu mara moja kwa mpinzani wake.
Azam FC iliyocheza vizuri kwenye mchezo huo kama ilivyo kwa KCCA, ilibidi isubiri hadi dakika ya 90 kuweza kuandika bao la kusawazisha lililofungwa na winga wa kulia anayechipukia Idd Kipagwile, kwa njia ya mkwaju wa moja kwa moja wa adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la 18 uliomgonja kipa kabla ya kutinga wavuni.
KCCA ilitangulia kupata bao dakika ya 74 lilofungwa na kiungo Bukenya Lawrence, kwa shuti kali nje ya eneo la 18 lililomshinda kipa wa Azam FC, Razak Abalora, aliyekuwa akicheza mechi yake ya tatu tokea asajiliwe na timu hiyo akitokea WAFA SC ya Ghana.
Kocha Mkuu wa Azam FC, alibadilisha wachezaji katika maeneo ya kiungo na ushambuliaji, kipindi cha kwanza akianza na washambuliaji Yahya Zayd, Wazir Junior, viungo Frank Domayo, Nahodha Himid Mao, Braison Raphael.
Kipindi cha pili katika dakika tofauti Yahaya Mohammed, Enock Atta, Masoud Abdallah, Idd Kipagwile, Ramadhan Singano, Stephan Kingue, walichukua nafasi zao, lakini timu ilionekana kucheza kwa ubora ule ule na hatimaye kupata bao la kusawazisha kwenye dakika ya pili ya nyongeza kati ya tatu zilizoongezwa baada ya kumalizika dakika 90.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kucheza mchezo wa pili wa kirafiki kesho Ijumaa dhidi ya URA utakaofanyika Uwanja wa Phillip Omondi saa 10.00 jioni.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:
Razak Abalora, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Himid Mao (C)/Kingue dk 81, Braison Raphael/Masoud dk 46, Salum Abubakar/Kipagwile dk 84, Yahya Zayd/Yahaya dk 46, Wazir Junior/Atta dk 78, Frank Domayo/Singano dk 80.

Maoni