MAYANGA KUITUMIA MECHI YA BOTSWANA, KUTENGENEZA KIKOSI CHA AFCON

Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania Salum Mayanga amefunguka kuwa mchezo wao dhidi ya Botswana ni mchezo ambao utawasaidia kwa namna moja ama nyingine katika kutengeneza kikosi ambacho kitashiriki katika hatua ya kufuzu katika mashindano ya Afcon.
Mayanga alisema mechi hiyo ina umuhimu mkubwa katika timu hiyo kutokana itakuwa ni kipimo kwao, pia kitatoa taswira ya kikosi ambacho kitaenda kucheza mechi za kufuzu katika fainali za Afcon.
“Siyo mechi ya kuibeza kwetu hii kwa sababu ni mechi kubwa mno, ambayo inatoa taswira katika kikosi chte kwasababu tutakuwa na mechi kama tatu za namna hii hivyo itatusaidia kutengeneza kikosi ambacho kitaenda kwenye mashindano ya kufuzu ya Afcon”, alisema.
Akizungumzia kuhusu kuwa na rekodi nzuri tangu akiichukua timu hiyo, alisema kuwa ni lengo lao kuendeleza rekodi hiyo ili timu ifanye vizuri, lakini pia alisisitiza kuwa kuna mipango waliyopanga na benchi la ufundi ili wafanye vizuri.
“Nilishaongea na wenzangu kuhusu hili jambo, na uzuri ni kwamba wote wanatambua kuwa hawataki kupoteza mchezo wowote ili kulinda heshima yetu ya kutokufungwa, lakini tumejipanga kiufundi ili tuweze kufanya vizuri zaidi tukiwa na vijana wetu,”alisena.
Mayanga aliongeza kuwa pia mechi hiyo wanatarajia kufanya vizuri ili kujiweka katika nafasi nzuri za Fifa kutokana na mechi hiyo kuwa katika kalenda ya Fifa hivyo kufanya kwao vizuri kutaipandisha timu kwenye nafasi hizo.

Maoni