Nilitaka kujiua nilipokuwa ICU - Cjamoker

Cjamoker amebainisha hayo leo wakati alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha Planet Bongo kutoka East Africa Radio baada ya kuulizwa swali na mmoja wa waongozaji wa kipindi hicho kuhusiana na maisha yake aliyoyapitia katika kuumwa.
"Nilitaka kujiua nilipokuwa ICU, maana kuna siku nilikuwa naota ndoto kama hospitali imevamiwa na madudu halafu yakawa yanauwa 'Nurse' sasa mimi kwa kutaka kujiokoa nikajikuta najitoa mipira niliyokuwa nimewekewa kunisaidia kupumua na kusababisha hali ya taharuki kwa madaktari pindi walipokuja, kwani madaktari hao baadhi yao walikuwa hawawezi namna ya kuirudisha mipira hiyo hivyo ilibidi waniwekee dripu la kawaida mpaka asubuhi ndipo nilipokuja kuwekewa mipira hiyo na madaktari wengine", amesema Cjamoker.
Pamoja na hayo, Cjamoker ameweka wazi jambo ambalo lilimpelekea kuumwa kwa kipindi kirefu na kushindwa kufanya kazi ya aina yoyote ile na mwisho kuwa mtu wa kulala tu.
“Kitu kilichokuja kunisababishia mimi kuumwa ni kutokula kwa wakati, nilikuwa napitiliza kutokula kwa wakati, unajua kazi zangu ni production nakuwa busy, wakaniambia utumbo umetoboka, umejikunja na pia waligundua na henia, pia wakaniambia matumizi ya pombe ingawa nilikuwa situmii sana”, alisema Cjamoker.
Kwa upande mwingine, Cjamoker amesema anawashukuru wazazi wake kwa upendo waliyokuwa wamemuonyesha wakati alipokuwa yupo kitandani kwa maana kuna vitu vingine alikuwa hawezi kuvifanya yeye kama yeye.

Maoni