Shaaban kwenda Sauzi kufanyiwa uchunguzi

MSHAMBULIAJI kinda wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shaaban Idd, anatarajia kuondoka nchini kesho Ijumaa kuelekea nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi wa afya yake.
Hii ni mara ya pili kwa nyota huyo kupelekwa nchini humo kwa matibabu kutokana na tatizo la misuli ya nyama za paja inayomsumbua, awali mwezi uliopita alikwenda na daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, sambamba na mshambuliaji Mbaraka Yusuph.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa kwanza katika Hospitali ya Muelmed, iliyopo jijini Pretoria, nchini humo, Idd alitakiwa akae nje ya dimba takribani mwezi mmoja, lakini baada ya muda huo kupita na kuanza mazoezi mepesi kama alivyoamuriwa bado afya yake imeshindwa kurejea vizuri hali inayoilazima Azam FC kumrudisha tena huko.
Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, ameuambia mtandao rasmi wa klabu
www.azamfc.co.tz kuwa, Idd ataongozana na Meneja Mkuu, Abdul Mohamed, katika safari yake hiyo ili kuhakikisha anakuwa kwenye uangalizi mzuri.
“Bado hali yake haijatengamaa na alianza mazoezi mepesi mepesi tukitarajia pengine angerejea kwenye hali yake lakini mpaka sasa ninavyoongea hali yake haijakuwa vizuri, kwa hiyo bado Azam FC inaangalia ni kwa jinsi gani ya kuweza kumsaidia mchezaji huyu ili aweze kurudi kwenye timu yake ya Azam FC akiwa mzima na kutoa mchango wake.
“Uongozi wa Azam FC umechukua jukumu la kumsafirisha mchezaji huyu kwenda jijini Pretoria Afrika Kusini kwa matibabu na anatarajia kuondoka nchini kesho (Ijumaa), ni mchezaji ambaye tunamhitaji kwenye timu na ligi inatarajia kuanza kwa hiyo uongozi umefanya kazi ya ziada ya kumpeleka mchezaji huyu Afrika Kusini kwa matibabu ili aweze kupona na kurejea uwanjani na kujiunga na wenzake, ni mchezaji mwenye mchango mkubwa kila mmoja anafahamu,” alisema.
Wakati huo huo, Idd alisema Azam FC inatarajia kuanza mazoezi kesho Ijumaa saa 10.00 jioni tayari kabisa kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kwenda kuvaana na Ndanda Agosti 26 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
“Tunatarajia mchezo huo utakuwa na upinzani na vile vile Ndanda ni timu nzuri, wenzetu Ndanda wanajitahidi wakiwa kwao lakini tunahitaji kwenda tuanze ugenini kwa ushindi, kwa hiyo ushindi haupatikani bila maandalizi, na maandalizi ya mwisho yataanza kesho,” alisema.
Aidha kabla ya kikosi kuelekea mkoani Mtwara Jumatano ijayo Agosti 23, Idd alisema kitacheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya timu ya vijana ya kikosi hicho Azam FC U-20, utakaofanyika uwanja wa nyasi za kawaida kwenye makao makuu ya timu hiyo Azam Complex Agosti 22 mwaka huu.

Maoni