SIMBA KUCHEZA NA SINGIDA UNITED TAIFA JUMAPILI MECHI YA KIRAFIKI

KIKOSI cha Simba SC kinatarajiwa kuteremka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumapili kumenyana na Singida United katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wa jadi, Yanga Agosti 23 mwaka huu.
Huo utakuwa mchezo wa nne wa kirafiki kujiandaa na msimu mpya kwa kikosi cha kocha Mcaameroon, Joseph Marius Omog baada ya awaki kushinda mechi moja, sare moja na kufungwa katika mechi zake tatu zilizotangulia.
Na utakuwa mchezo wa kwanza kucheza naa timu ya nyumbani, kwani mechi zilizopita ilifungwa 1-0 na wenyeji Orlando Pirates kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Bidvest katika ziara ya Afrika Kusini na Jumanne ikashinda 1-0 dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda Uwanja wa Taifa.

Kwa Singida United itakuwa inacheza mechi ya pili ndani ya wiki moja Uwanja wa Taifa, kwani Jumamosi iliyopita ilifungwa 3-2 na mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania, Yanga licha ya kuongoza kwa mabao 2-1 hadi mapumziko.
Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm anaamini kucheza na vigogo wa Tanzania, Simba na Yanga kabla ya kuingia kwenye Ligi Kuu ni kipimo kizuri na Jumamosi atakamilisha mpango wake.
Pamoja na kwamba imepanda Ligi Kuu msimu huu, lakini Singida United inatarajiwa kufanya vizuri katika ligi hiyo baada ya usajili wa wachezaji nyota kutoka mbalimbali maarufu, wakiwemo wa saba wa kigeni.

Maoni