StarTimes RBA yaja na mechi ya kipekee

Wadhamini wakuu wa ligi ya kikapu ya RBA, kampuni ya StarMedia Tanzania Limited sasa wameleta mechi ya All Star ambayo itashirikisha wachezaji vinara katika ligi hiyo.

Mechi ya All Star inatarajiwa kuchezwa siku ya Jumamosi tarehe 2 mwezi wa tisa.
Baada ya kuanza kwa hatua ya robo fainali (playoffs), wapenzi wa mpira wa kikapu jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla watapata nafasi ya kushuhudia wachezaji vinara wa ligi hiyo wakiwapatia burudani Stahiki kupitia mchezo wa All Stars.

Mchezo utahusisha timu mbili ambazo zimepewa majina ya NYOTA na MAMBO, majina ya vifurushi vya gharama nafuu vya StarTimes, ndizo zitashuka dimbani katika uwanja wa Ndani wa Taifa ili kutoa Burudani ya aina yake kwa watazamaji.

Mchezo unatarajiwa kupigwa kati ya saa 2 hadi saa 4 Usiku, Lakini kabla ya mchezo kuanza kutakuwa na michezo kadhaa ya utangulizi na Onyesho kutoka kwa Msanii Jay Moe.

Mchezo wa All Star ni sehemu ya ufunguzi kwa hatua ya Mtoano (PlayOffs) ambayo itahusisha jumla ya timu nane (8), ili kumpata mshindi na timu tatu (3) zitakazopata nafasi ya kushiriki ligi ya Taifa hapo baadaye mwaka huu. Hatua hiyo inatarajiwa kuanza tarehe 6 Septemba.

Akizungumzia muendelezo wa ligi hiyo Meneja Mahusiano wa Kampuni ya StarTimes, Ndg. Juma Suluhu amesema kuwa kampuni hiyo itaendelea kusaidia ukuaji wa michezo nchini ikiwa ni sehemu ya Uhusiano mzuri kati ya kampuni hiyo na Watanzania.

“Tunajisikia fahari kuchangia kuinua vipaji kwa vijana wa kitanzania kupitia mpira wa kikapu ambao pia una wapenzi na washiriki wengi hivyo udhamini wetu unakuwa ni sehemu ya shughuli nyingi za kijamii ambazo kampuni yetu inaendelea kufanya” alisema Juma.

Ligi ya StarTimes RBA inaonyeshwa MUBASHARA kila siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kupitia Chaneli ya Sibuka Maisha ambayo inapatikana katika king’amuzi cha Startimes, kwa gharama ya Tshs 3000 kwa mwezi.

Mbali na ligi RBA StarTimes ndiyo kampuni yenye kibali cha kuonyesha michuano ya Mpira wa kikapu Kimataifa (FIBA), na sasa wanaendelea kuonyesha ligi ya Kikapu kwa Wanawake AfroBasket inayochezwa nchini Mali.

Maoni