Vijana na Kiswahili

Vijana na Kiswahili ni suala la msingi katika kudumisha na kustawisha lugha hiyo kama nyingine yoyote.
Katika taifa lolote vijana ndio chachu ya
maendeleo . Barani Afrika, ikiwa pamoja na
Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla, kuna
idadi kubwa ya vijana ambao ndio wanaotegemewa zaidi na taifa lao. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba pengine vijana hao hawana uzalendo na lugha yao ya taifa kama vile Kiswahili. Hii ni kutokana na kuonekana wazi kuwa lugha ya Kiswahili haipewi kipaumbele ukilinganisha na lugha nyingine, hasa lugha za kigeni.
Hili janga linatokana na vijana kujiona wamestaarabika kwa kupata elimu ya kutoka kwa watu wa magharibi inayofundishwa kwa lugha za kigeni na hivyo kujikuta wanaidharau lugha ya nchi yao wenyewe. Ndiyo chanzo cha ukasumba ndani ya nchi. Kwa kuwa vijana ndio wanaopata elimu hii, hawana budi kukaa na kuchambua yaliyo mema na kuyafanyia kazi na ndiyo maana inawezekana kusema vijana ndiyo chanzo cha kudumaza lugha ya Kiswahili kwa sababu zifuatazo;
1. Elimu
Elimu wanayoipata wanafundishwa kwa kutumia lugha za kigeni, hasa kwa wanafunzi wa shule za sekondari , maana mitaala yao mingi inatumia lugha ya Kiingereza na hivyo lugha ya Kiswahili kuonekana haina tija.
2. Utawala
Utawala ndio unahusika na kuandaa vijana kwa kutoa elimu inayodumaza lugha ya Kiswahili kwa kutokufanyia mabadiliko ya mitaala ya elimu kwa ngazi za elimu ya sekondari na vyuo, maana ndio hutoa vijana wanaokuwa na ukasumba na lugha yao ya Kiswahili kwa sababu tofautitofauti wanazojaribu kuzitoa.
3. Maendeleo ya sayansi na teknolojia
Hii husababishwa na vijana wengi ambao hujiona kama hawakustahili kuwa na lugha ya Kiswahili kutokana na mazoea ya kutumia mambo yaliyotumiwa au yaliyofanywa na yanayofanywa na wageni ambao kwa namna moja ama nyingine wamewaathiri vijana wazawa ambao sasa wanaona ndio msingi wa
maisha yao ya kila siku.
4. Matumizi ya misimu
Misimu mingi itumiwayo na vijana wengi huwa si sanifu na huwa imechukua maneno mengi kutoka katika lugha za kigeni ambazo hazina sarufi inayofanana na ile ya lugha ya Kiswahili.
5. Vyombo vya mawasiliano
Vyombo vya mawasiliano , kwa mfano simu , vimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza ambayo ndio lugha wanayotumia wanafunzi wote wa shule za sekondari na vyuo.
6. Vijana kutokubali mabadiliko
Vijana walio wengi huwa hawako tayari kupokea mabadiliko; kwa mfano: wanapokuwa
mahakamani ambako sheria nyingi zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, huwa hazifanyii mabadiliko yoyote ya lugha yao.

Maoni