Wafanyabiashara Kenya wawaomba wananchi kurejea kazini

Muungano wa wafanyibiashara Kenya KEPSA umetoa wito kwa Wakenya kurejea kazini na kuendelea na biashara zao.
Siku tatu baada ya uchaguzi, taharuki imetanda katika baadhi ya maeneo ingawa utulivu umedumu katika taifa hilo. Maelfu ya wakenya waliosafiri kupiga kura nje ya baadhi ya maeneo wamekwama huku wamiliki wa magari wakihofia uharibifu wa magari hayo.
Hata hivyo, wafanyibiashara hao wakiongozwa na mwenyekiti wao, Vimal Shah, wamewataka Wakenya kutotiwa wasiwasi na ujumlishaji wa matokeo unaoendelea na badala yake kuwa na ujasiri wa kuendelea na shughuli zao.
“Turejee katika shughuli za kawaida, tusijifungie majumba,” alisema. Bwana Shah ametoa wito kwa tume ya IEBC kuwasilisha matokeo kuondoa wasiwasi.
“Tunawaomba wahusika waweze kutekeleza majukumu yao bila wasiwasi na kuwa na usawa na haki kwa wote,” aliongeza.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa muungano wa wamiliki wa magari ya usafiri, maarufu matatu, Simon Kimutai, amewarai waajiriwa sehemu tofauti kujitokeza wamiliki wa magari kuyaruhusu magari.

Maoni