WANASOKA 10 WENYE KASI ZAIDI DUNIANI 2017

Mirror wamewahi kuripoti juu utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na klabu moja ya huko Mexico, C.F. Pachuca uliofichua wanasoka 10 wenye kasi zaidi duniani. Wapo wachezaji ambao usingewatarajia kuwemo kwenye orodha hii. Gareth Bale pamoja na mchezaji bora wa Ulaya Cristiano Ronaldo wamo kwenye pamoja na mpinzani wao wa La Liga Lionel Messi.
Mshangao mkubwa uliopo kwenye orodha hii ni uwepo wa mchezaji wa Everton, Wayne Rooney. Yumo pia nyota mwenzie wa Everton Aaron Lenon. Mbali na wachezaji wa EPL, La Liga na Bundesliga orodha hii inao pia nyota kutoka Ligi Kuu ya Brazil na ile ya Mexico. Hii hapa 10 bora;
10) Wayne Rooney (Everton)
Mfungaji bora huyu wa muda wote wa timu ya taifa ya England pamoja na klabu ya Manchester United yumo kwenye orodha hii akitajwa kuwa na kasi ya kilomita 31.2 kwa saa. Inashangaza yeye kuwepo hapa kwa kuwa kwenye miaka ya karibuni amekuwa haonekani akiwa na kasi ya namna hiyo na hata kiwango chake kwa ujumla kuonekana kuporomoka.
9) Lionel Messi (Barcelona)
Unaweza kuongoza kwenye kushinda tuzo ya Balon d’or mara nyingi zaidi lakini Antonio Valencia akakuacha mbali mno kwenye takwimu za kuwa na kasi uwanjani. Messi ametajwa kuwa na kasi ya kilomita 32.5 kwa saa. Hiyo ni kasi ya hatari mno kwa mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kukokota mpira na ndio maana walinzi hupata tabu mno kumzuia.
8 Theo Walcott (Arsenal)
Nyota huyu wa Arsenal anafahamika kwa kasi uwanjani. Lakini anaishia kukamata nagasi ya 8 kwenye orodha hii akiripotiwa kuwa na kasi ya kilomita 32.7 kwa saa. Kasi ndio silaha kuu ya winga huyo awapo uwanjani na ndio mchezaji mwenye kasi zaidi kwenye klabu ya Arsenal ingawa mlinzi wa kulia Hector Bellerin kwa sasa anachuana naye kwenye nafasi hiyo.
7) Cristiano Ronaldo (Real Madrid)
Mshindi huyu wa tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya tayari ana miaka 32 lakini bado anaweza kukimbia kwa kasi mno uwanjani. Ronaldo huwa hapendi kuvaa viatu vyeusi awapo uwanjani kwa kile alichokitaja kuwa rangi nyeusi ni rangi ya mwendo wa taratibu na yeye hutaka ajione mwenye kasi uwanjani. Uchunguzi umemtaja kuwa na kasi ya kilomita 33.6 kwa saa.
6) Aaaron Lennon (Everton)
Lenon anafahamika kwa kuwa na kasi ya ajabu lakini siku hizi amekuwa hapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha mwalimu Ronald Koeman. Hata hivyo takwimu za uchunguzi huu zimebaini kwamba yeye ndiye mchezaji Muingereza mwenye kasi zaidi uwanjani akitajwa kuwa na kasi ya kilomita 33.8 kwa saa.
5) Pierre-Emerick Aubameyang (Borussia Dortmund)
Inashangaza mshambuliaji huyu kutoka Gabon hayumo angalau kwenye tatu bora kwenye orodha hii. Hata hivyo sio mbaya kuwemo kwenye nafasi ya tano kwa kuwa wamo wengine wanaosifika lakini hawakuweza kukanyaga kwenye kumi bora. Aubameyang anatajwa kuwa na klasi ya kilomita 34.6 kwa saa.
4) Antonio Valencia (Manchester United)
Jose Mourinho anamtaja mchezaji wake huyu kuwa ni mlinzi bora zaidi wa kulia duniani. Huenda watu wengi hawawezi kukubaliana na maneno ya Jose Mourinho. Lakini wengi wanakubali kuwa Valnencia ni tishio mno linapokuja swala la kukimbia. Anayo kasi ya kilomita 35.1 kwa saa uwanjani kwa mujibu wa uchunguzi huu.
3) Jurgen Damm (Tigres UANL)
Tunaweza kuwa hatumfahamu Damm. Lakini uchunguzi huu unamtambua kama mchezaji mwenye kasi zaidi duniani akizidiwa na watu wawili pekee. Kiungo huyu raia wa Mexico anatajwa kuwa na kasi ya kilomita 35.2 kwa saa. Ni yeye pekee anayetokea Ligi Kuu ya Mexico kwenye orodha hii.
2) Orlando Berrio (Flamengo)
Ni jina ambalo wengi wetu hatujawahi kulisikia kabla lakini raia huyu wa Colombia anawaacha mbali Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kwenye swala la kasi uwanjani kwa mujibu wa utafiti uliofanywa. Mchezaji huyu wa Flamengo ya Brazil anatajwa kuwa na kasi ya kilomita 36 kwa saa.
1) Gareth Bale (Real Madrid)
Haishangazi winga huyu wa Real Madrid kuwa juu zaidi kwenye orodha hii. Hatuwezi kusahau namna alivyomfanya Marc Bartra akiwa Barcelona kuonekana kana kwamba alikuwa anatembea wakati wakishindana kuukimbilia mpira kwenye fainali ya Kombe la Mfalme la mwaka 2014. Bale anatajwa kuwa na kasi ya kilomita 36.9 kwa saa.

Maoni