"MBALAMWEZI YA KISWAHILI" : Fasihi ni mwarobaini wa matatizo ya kiafya

By Erasto Duwe
Wanajamii katika maisha yao ya kila siku hukutana na mambo mazuri na kwa upande mwingine matatizo ambayo hukatisha tamaa.
Matatizo hayo ni kama vile magonjwa, kufiwa, umaskini na kufukuzwa kazi. Mengine ni kutengwa, kukataliwa, kunyanyapaliwa, migogoro ya ndoa, kuonewa, kunyanyaswa na kukandamizwa.
Hayo na mengine aghalabu husababisha msongo wa mawazo ambao matokeo yake ni shinikizo la damu, matatizo ya moyo, kiharusi na wendawazimu ikiwa anayekabiliwa nayo hatachukua hatua mwafaka za kuyatanzua.
Matatizo katika maisha hayaepukiki wala hayakimbiwi. Jambo la msingi ni kuweka mikakati ya kukabiliana nayo pindi yanapotokea.
Wasanii wengi wa kazi za kifasihi, wamekuwa wakiwachora wahusika wao wakikabiliwa na matatizo mbalimbali makubwa. Kwa kadiri ya makusudio ya msanii wa kazi husika, wapo wahusika wanaopambana na matatizo hayo na kuyashinda hata kama ni makubwa kiasi gani.
Katika jamii tuishiyo, kila mwanajamii kwa wakati wake hukabiliwa na matatizo mbalimbali. Uwezo wa kukabiliana na matatizo hayo, hutofautiana kati ya mwanajamii mmoja na mwingine. Matatizo hayo yasipokabiliwa kwa haraka na kutatuliwa, huweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya kwa mhusika au wahusika.
Katika jamii zenye mapenzi makubwa ya usomaji wa kazi za kifasihi hususan riwaya, imebainika kuwa, riwaya hizo zimekuwa ‘mwarobaini’ kwa wasomaji wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali. Dk Ernesta Mosha wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anabainisha kuwa, katika jamii za Kimagharibi watu wenye mapenzi makubwa ya usomaji wa riwaya ambao wamewahi kukabiliwa na matatizo mazito maishani, wamekiri kwamba, riwaya zimewasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na matatizo yao.
Anaeleza kuwa, watu hao badala ya kujidhuru au kukata tamaa kutokana na matatizo yaliyowakabili, riwaya zimewasaidia kutatua matatizo hayo.
Hii ni kwa sababu ijapokuwa riwaya ni kazi ya kisanaa, aghalabu huwa na visa na matukio ambayo hurandana barabara na yale yatokeayo katika maisha yetu ya kila siku. Mtu anapokabiliwa na tatizo fulani, akisoma riwaya na kuona kuwa kuna mhusika au wahusika wanaokabiliwa na matatizo kama yake au yanayozidi kwa uzito matatizo yake na kuona jinsi yalivyotatuliwa; msomaji hupata mbinu za kutatua matatizo yanayomkabili.
Hata hivyo, hali ya kubaini kwamba kuna watu wengine wenye matatizo makubwa na wakamudu kuyatatua, hutoa nafasi ya kupata ahueni, kujitafakari na kutatua matatizo hayo kwa njia stahiki.
Halikadhalika, kupitia wahusika wa riwaya waliojidhuru au kuathirika na matatizo yaliyowakabili, hutupatia fursa ya kujifunza athari za kujidhuru huko na matatizo yanayojitokeza kwa wategemezi wao.
Riwaya za kisaikolojia ni aina ya riwaya zinazoweza kutoa mwarobaini kwa matatizo ya namna hii. Profesa Mulokozi anaeleza kuwa, hizi ni riwaya zinazododosa nafsi ya mhusika: fikra, hisia, mawazo, imani, hofu, mashaka, matumaini na matamanio yake binafsi na athari za mambo hayo kwake na kwa jamii.
Baadhi ya riwaya zinazoingia katika mkondo huu ni Rosa Mistika, Kichwamaji (E. Kezilahabi), Nyota ya Rehema, Tata za Asumini (S. Mohamed), Msimu wa Vipepeo (K. Wamitila) na nyinginezo.
Wapenzi wasomaji wa Mbalamwezi ya Kiswahili, tujenge tabia ya kujisomea riwaya za Kiswahili hususan za kisaikolojia. Hizi hutoa mafunzo makubwa kuhusu matatizo yanayotukabili maishani.

Maoni