Azam FC yaifunza soka Lipuli, yaidunga 1-0

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendelea kufanya kweli kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Lipuli bao 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam leo usiku.
Kwa ushindi huo Azam FC imefanikiwa kuikamata Mtibwa Sugar baada ya kufikisha jumla ya pointi 10 zikiwa zinalingana kileleni huku ikiwa timu pekee ambayo haijaruhusu bao lolote tokea ligi hiyo ilipoanza Agosti 26 mwaka huu.
Bao pekee la Azam FC limefungwa na Mbaraka Yusuph dakika ya 11 akipokea pasi safi ya nahodha Himid Mao ‘Ninja’, likiwa ni bao lake la pili kwenye mechi ya pili mfululizo lingine akiitungua timu yake ya zamani Kagera Sugar katika ushindi wa 1-0.
Licha ya kufunga bao hilo, Azam FC ilifanikiwa kutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa na kutengeneza nafasi nyingi takribani 10 ambazo hazikutumiwa vema.
Lakini safu ya ushambuliaji ilikuwa ikiundwa na wachezaji vijana Yahya Zayd na Yusuph, ambao wanaendelea kujifunza mikikimikiki ya ligi hiyo,
Kabla ya mchezo huo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, alipata fursa ya kuwakabishi tuzo za wachezaji bora wa Azam FC mwezi Agosti, beki Yakubu Mohammed, akitwaa kwa upande wa timu kubwa na kiungo Twaha Ahmed, akibeba ya timu ndogo (Azam B).
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho Jumatatu kanla ya kuanza mazoezi Jumanne kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Singida United, uutakaofanyika Uwanja wa Jamhuri Dodoma Septemba 30 mwaka huu.
Kikosi cha Azam FC leo
Razak Abalora, Himid Mao, Bruce Kangwa, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Daniel Amoah, Stephan Kingue/Braison Raphael dk 59, Frank Domayo, Salum Abubakar, Yahya Zayd/Wazir Junior dk 59, Mbaraka Yusuph/Yahaya Mohammed dk 79.

Maoni