Maboresho hospitali ya Muhimbili yanatia moyo

HABARI kwamba Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ya jijini Dar es Salaam, imelaza viongozi 17 wa Serikali ya Awamu hii ya Tano wakiwa mahututi kwa magonjwa badala ya kuwakimbizia nje ya nchi, inatia moyo sana.
Taarifa hii ya kutia moyo iliandikiwa na gazeti hili jana kutokana na mahojiano na Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Neema Mwangomo juu ya mwamko wa viongozi wa kutibiwa katika hospitali hiyo.
Mwangomo anasema idadi hiyo ni kwa watendaji wakuu wa serikali, lakini pia kuna idadi kubwa ya familia zao na watu wengine mashuhuri, ambao nao wanatibiwa katika wodi hiyo.
Hii imewezekana kutokana na maboresho yaliyofanywa kwa kiasi kikubwa hospitalini hapo, ikiwa ni pamoja na kutenga wodi maalumu kwa ajili ya viongozi hawa kama alivyoeleza Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru mwanzoni mwa mwaka huu.
Museru akasema kwa muda mrefu hospitali hiyo ilikuwa haina sehemu maalumu na yenye hadhi kwa ajili ya kuwapokea viongozi hao na watu mashuhuri kwa ajili ya matibabu. Akasisitiza kwamba ili kupunguza changamoto hiyo katika mpango wa muda mfupi, hospitali ikabadilisha Wodi Namba 18 ya Sewa Haji na kuifanyia ukarabati mkubwa ili kupata vyumba vizuri vya kulaza wagonjwa hao.
Hii ni habari njema. Kutengwa kwa wodi hiyo, sasa kunaokoa mamilioni ya fedha ambazo viongozi walikuwa wakitumia kwenda nje ya nchi kutibiwa. Ndio maana, kwa sasa kama taifa, tunaona fahari kubwa kwa kuwa hakuna haja viongozi wa ngazi mbalimbali kukimbilia nje wakati hospitali yetu ya taifa ina uwezo huo.
Pia huduma kwa wagonjwa zimeongezeka kiasi cha kuwezesha wagonjwa 238,026 kutibiwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2016, ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa 191,241 waliohudumiwa kati ya Julai na Desemba 2015, hivyo kufanya ongezeko la wagonjwa 46,785 ambao ni sawa na asilimia 20 kwa mujibu wa Mwangomo.
Tunamshukuru Rais John Magufuli kutokana na busara zake za kubana matumizi ambapo mpango wake wa kuboresha huduma, kumewezesha kupunguza gharama kubwa ambazo zinarudi katika mzungumko wa matumizi ya maendeleo kwa manufaa ya Watanzania.
Ni kutokana na uamuzi wake huo, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Afya kwa pamoja zikatoa mwongozo wa namna ya kiongozi kwenda nje ya nchi, kwa kusema ni lazima kiongozi huyo awe na matatizo ya kiafya, ambayo matibabu yake hayapatikani nchini.

Maoni