MGHANA WA SIMBA AIWAHI AZAM FC

KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amefarijika baada ya kupewa taarifa za kurejea nchini kwa mshambuliaji wake wa kimataifa Mghana, Nicholaus Gyan aliyedumu na kikosi cha timu hiyo kwa muda wa siku moja kisha akaondoka zake.

Gyan ambaye amesajiliwa na Simba hivi karibuni akitokea Ghana, awali alitua nchini siku moja kabla ya Tamasha la Simba Day na baada ya tamasha hilo aliondoka zake.

Kuondoka kwake huko nchini na kurudi kwao Ghana kuliwashtua vilivyo mashabiki wengi wa timu hiyo, lakini pia Omog ambaye tayari alikuwa ameishamweka katika mipango yake kwa ajili ya mechi ya Ngoa ya Jamii dhidi Yanga iliyochezwa Agosti 23 ili aweze kuiongoza timu yake hiyo kuibuka na ushindi.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Omog alisema kuwa amepewa taarifa kuwa Gyan anatarajiwa kutua nchini leo Ijumaa tayari kwa kujifua kwa ajili ya mechi ijayo ya ligi kuu dhidi ya Azam FC.

Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, itapigwa Jumatano ijayo ya Septemba 6 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

“Kama atatua kweli ni jambo zuri kwetu kwani ataiongezea nguvu safu yetu ya ushambuliaji kwa ajili ya kukabiliana na Azam.
“Gyan yupo vizuri, alionyesha uwezo mkubwa tulipocheza na Rayon Sports ya Rwanda siku ya Simba Day, kwa hiyo ni matumaini yangu atatusaidia katika mechi hiyo na nyingine zinazokuja,” alisema Omog.

CHANZO: CHAMPIONI.

Maoni