VAN DER SAR BADO ANAKUMBUKA “KAZI KAZI YA KOCHA ALEX FERGUSON



Na Saleh Ally aliyekuwa Manchester

KIPA Edwin van der Sar ana rekodi ya kuwa mmoja wa wachezaji wawili wenye umri wa miaka 40 kucheza katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yaani Champions League Final.

Amecheza soka la kulipwa kwa miaka 26 na alifanikiwa kufunga bao moja tu la mkwaju wa penalti wakati akiwa Ajax ambayo aliichezea mechi 226 na kufanikiwa kubeba makombe kadhaa yakiwemo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kipa huyo ambaye ni mmoja wa makipa warefu zaidi duniani amecheza mechi 313 akiwa na timu za Ligi Kuu England, yaani Fulham na baadaye Manchester United.

Katika mahojiano aliyofanyiwa kwa pamoja na runinga ya Manchester United, runinga ya FC Barcelona na Gazeti la Championi, anasema wakati akitua Fulham mwaka 2001 akitokea Juventus, alijua siku moja angeichezea Manchester United.



“Bila ya hofu nilijua hilo litafanyika siku moja. Unajua Kocha (Sir) Alex Ferguson aliwahi kuniuliza mara kadhaa kama nilikuwa ninaweza kwenda England.

“Lakini awali sikupenda kuondoka Ajax, nilitaka kubaki pale kabla ya kubadili mawazo na kwenda Italia ambako sikufurahia sana, nikaona ni vizuri kwenda England kwa kuwa kuna ushindani pia nilitaka kuinua kiwango changu.

“Ningekuwa na subira ningeweza kusubiri niende katika klabu kubwa. Lakini nilikuwa nina malengo ambayo wengi hawakujua. Unapokuwa katika klabu ndogo, unapokea mashambulizi mengi zaidi.


“Ukiwa unakutana na mashambulizi mengi ni rahisi kujipanga na kujiweka fiti zaidi. Nilijua ningeenda timu kubwa baadaye baada ya kuwa fiti hasa. Kabla timu kubwa zilinihitaji lakini niliamua kubaki Fulham zaidi kwa kuwa nilifurahia maisha ya pale. Mwisho niliamua kuondoka na

kwenda Manchester United,” anasema Van Der Sar.

Alipoulizwa kuhusiana na Ferguson na uongozi wake ulivyo kama kuna tofauti na makocha wengi, anasema:

“Ferguson ni kocha wa aina yake, hauwezi kumfananisha na makocha karibu wote duniani. Nimefundishwa na makocha wengi ambao walinisaidia kufika nilipo sasa lakini yeye (Ferguson), alikuwa anafanya mambo

mengi tofauti na wengine.


“Nilichovutiwa zaidi kwake ni suala la nidhamu na kamwe hakuwa muoga hata mchezaji aliyekuwa staa kupita wote, alitakiwa kufuata utaratibu kama wengine na ikiwezekana kumsikiliza anachoelekeza.

“Ndani ya Manchester United, kama ni kwenye timu mkubwa kuliko wote ni kocha na anafuatia kocha msaidizi na wengine wa benchi la ufundi.

Heshima ni kubwa hata kwa wale wanaotunza vifaa. Ukionyesha dharau, basi ujue utakwenda na hautakuwa na nafasi.

“Lakini ni mtu ambaye pamoja na ufundi, uwezo wa maneno yake ya taratibu huku akiwa amekukazia macho, lazima utabadilika na utataka kupigana na kushinda,” anasema na kuongeza:

“Wakati mwingine anaweza kuingia vyumbani asiseme jambo, mwisho akawahoji kuwa mnachofanya ni sawa au si sawa. Sasa malizeni mechi tutaonana baada ya dakika tisini. Inawezekana wakati huo mlikuwa nyuma kwa bao moja au mawili. Baada ya dakika tisini mkirejea mmeshinda 3-2,

anacheka na kuwaambia wakati mwingine mnapenda utani lakini kumbe mnamuelewa. Anawatakia siku njema.”

Wakati mahojiano yakiendelea, Kocha Sir Alex Ferguson alipita na Van der Sar akasimamisha mahojiano na kusalimiana naye kwa sekunde kama 15 akionyesha hawakuonana kwa siku nyingi na baada ya hapo Ferguson akatupungia mkono na kuondoka.



Kuhusiana na mabeki kati ya aliofanya nao kazi, Van der Sar anasema wako wengi akiwemo Frank de Boer aliyekuwa pacha wa Ronald de Boer aliocheza nao Ajax, pia Winston Borgarde na Danny Blind aliyekuwa nahodha wa Ajax wakati huo na ndiye baba wa Daley Blind wa Manchester

United sasa, lakini kwa kizazi cha sasa anasema Rio Ferdinand anaweza kuwa bora zaidi.

“Kwa kipindi cha sasa, kweli sijaona. Alikuwa beki hasa ambaye ana uwezo wa kuzuia na kuituliza timu na washambulizi wote hatari walikuwa na hofu naye,” anasema.

Mahojiano hayakuwa marefu sana kwa kuwa wachezaji wanakuwa na haraka kuingia kwenye vyumba ambako walikuwa wakiitwa mmojammoja na tunafanya

nao mahojiano.

Maoni