Askari wa FFU amuua ‘mkewe’ kwa risasi benki

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Manyara, Konstebo Cosmas James (H.2443) anadaiwa kumuua mwanamke mmoja, anayedaiwa kuwa ni mpenzi wake aliyezaa naye, kwa kumfyatulia risasi nne, kichwani, kifuani na shingoni, alipokuwa lindoni katika moja ya matawi ya benki mjini Babati.
Tukio hilo ni la juzi jioni saa 12.30 katika jengo la Benki ya NMB Tawi la wilayani Babati, lililopo kwenye mtaa wa Usalama katika kata ya Bagara tarafa ya Babati, ambapo inadaiwa kuwa askari huyo alimuua Regina Daniel (23), mkulima na mkazi wa Ngarenaro.
Inadaiwa pia kuwa mwanamke huyo, alikuwa ni mpenzi au mtalaka wa mtuhumiwa huyo, lakini hasa akiwa ni mzazi mwenzake; na kwamba kilichompeleka marehemu pale lindoni kwa ‘mumewe’ waliyetengana, ni katika harakati zake za kudai fedha za matunzo ya mtoto wao, ambaye alikuwa akiishi na mama yake baada ya ‘baba’ kuwatelekeza.
Taarifa za Polisi mkoani Manyara, zinaeleza zaidi kuwa askari huyo, alikuwa kazini akilinda jengo hilo la Benki ya NMB mjini Babati, wakati marehemu alipomfuata na ghafla kukawa na mabishano makali, kabla ya mtuhumiwa kuchukua hatua ya kufyatua risasi.
Silaha iliyotumika kwenye mauaji hayo ya benki ni aina ya SMG yenye namba za usajili 55052756, mali ya Jeshi la Polisi la Tanzania. Maganda matatu ya risasi za bunduki hiyo, pia yaliokotwa kwenye eneo la tukio, ingawa uchunguzi wa awali ulionesha kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na matundu manne ya risasi, kwenye paji la uso, kifuani na shingoni.
Upelelezi wa awali ulifanywa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Babati, Maketi Msangi akisaidiana na Inspekta Msaidizi wa Polisi, Aloyce na tayari jalada la kesi ya mauaji hayo lenye namba BAB/ IR/3296/2017 limefunguliwa mjini Babati.
Mtuhumiwa, Konstebo Cosmas alikamatwa baada ya tukio hilo na anaendelea kuhojiwa na polisi, kuhusu tukio hilo, lililoushitua mji wa Babati na maeneo ya jirani. Mwili wa marehemu kwa sasa umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Babati ya Mrara, ukisubiri uchunguzi zaidi wa kitabibu.

Chanzo: Habarileo

Maoni