Kocha Mpya Simba Awaacha Midomo Wazi Mashabiki.



Kocha msaidizi wa Simba, Djuma Masoud amesema sikuja kufanya maajabu bali kusaidia ili timu isonge mbele na kuendelea kuwa namba moja kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, kauli iliyowaacha midomo wazi baadhi ya Mashabiki wa klabu ya Simba huku wakishindwa kuelewa nini sababu ya kujiunga na Simba kama hana msaada wowote.

Kocha huyo Mrundi Masous alitambulishwa jana Simba akichukua mikoba ya Mganda Jackson Mayanja aliejiondoa kuinoa timu hiyo kwa matatizo ya kifamilia.

Kocha huyo mwenye miaka 40, amekiri yeye ni mpole kiasi na pia mkali kwani huwa hapendi mtu achezee kazi yake kwani anachotaka  kutafuta riziki na timu isonge mbele.

"Siwezi kuahidi kuwa nitafanya nini  kwani kila kitu anapanga Mungu hivyo namuomba aniwezeshe kutumia ujuzi wangu pamoja na ushirikiano na kocha mkuu kuifanya Simba iwe ya kwanza mpaka ubingwa,” alisema msaidizi huyo wa kocha Joseph Omog.

"Sijaja kuleta maajabu ila nimekuja kusaidia kitu kidogo ambacho Mungu amenipa ili timu isonge mbele," alisema kocha huyo wa zamani wa Rayon Sports ya Rwanda.

Alisema yeye kuja kuwa kocha msaidizi Tanzania si jambo la kushangaza kwani Simba ni  klabu kubwa na anaitumia kama  shule ya kuzidi kusonga mbele.

"Watu wanaweza kushangaa Rwanda nilikuwa kocha mkuu na huku nimekuja kuwa msadizi, lakini wajue wakati nilianza nilianza chini na baadae nikasema nataka kupanda hivyo nikawa kocha mkuu, lakini Simba ni kama nimekuja kusoma kwani ni moja ya klabu kubwa hivyo kitu  kikubwa nataka nisogee mbele"alisema.

Maoni