Mahakama Yawahukumu Watu Wawili Miaka 30 Jela na Adhabu ya Viboko 12


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu watu wanne kifungo cha miaka 30 jela na adhabu ya kuchapwa viboko 12; viboko sita wakati wa kuingia na sita wakati wa kutoka kwa kosa la wizi wa kutumia silaha.

Waliohukumiwa ni Donald Nzweka, Michael Pascal, Ally Akili na Kurwa Mwakagenda.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Respicious Mwijage alisema hakuna shaka washtakiwa walishiriki kutenda kosa chini mwanga wa kutosha na kwamba washtakiwa walitambuliwa ipasavyo.

”Nimeridhika Jamhuri imethibiisha kosa bila kuacha shaka dhidi ya washtakiwa hivyo nawatia hatiani kwa kosa la kutumia silaha kama walivyoshtakiwa.”

Kwa pamoja July 7, 2013 maeneo ya Boko Magengeni, DSM washtakiwa waliiba simu nne aina ya Nokia Sumsung na Tecno zenye thamani ya Tsh Milioni 1,300,000, pesa taslimu Tsh 150,000, cheni za dhababu mbili zenye thamani ya Tsh 750,000, vyote vikiwa na thamani ya Tsh 2,050,000 mali ya Hobokela Mwakijambile.

Upande wa Mashtaka ulikuwa na mashahidi 11 na washtakiwa walijitetea wenyewe ambapo baada ya Hakimu kupitia ushahidi wa pande zote mbili Mahakama ilijiuliza kwamba kosa la kutumia silaha ili lithibitike Jamhuri wana wajibu wa kuthibitisha bila kuacha shaka kwamba washtakiwa kabla ya kutenda awe na kifaa hatari au wawe zaidi ya mmoja na kwamba baada ya tukio hilo walitumia nguvu kwa mtu aliyeporwa.

Katika shauri hilo, mlalamikaji na mashahidi wengine walieleza kuwa usiku wa July 7 majambazi walivunja mlango mkuu wa nyumba yao kwa kutumia bomu ambalo lilitambuliwa na Polisi kuwa baruti.

Alidai waliendelea kuvunja milango mingine na baadaye waliingia katika chumba walichokuwa wamekaa, wakiwa katika chumba hicho chenye mwanga, mshtakiwa wa nne alishika panga na alianza kuwapiga nalo kwa kutumia ubapa.

Aidha, Hakimu alisema kwa kuzingatia ushahidi huo hakuna shaka kwamba mashahidi waliweza kuwatambua  majambazi hao na kwamba ni washtakiwa katika kesi hiyo ambapo alisema kwa kuangalia maelezo yao waliyotoa Polisi yanaonyesha jinsi walivyoshiriki katika tukio na kwamba washtakiwa ndio walioiba vifaa hivyo kwa kutumia silaha kali.

Utetezi wa washtakiwa kwamba walikamatwa maeneo tofauti na kupelekwa Oyster bay Polisi na kupigwa na kunyanyaswa, Mahakama ilisema ushahidi huo hauaminiki na hauwezi kupewa uzito wowote.

Utetezi wa washtakiwa wa kukanusha kutenda kosa haukutikisa kwa aina yoyote ushahidi wa upande wa mashtaka.

”Nimeridhika na upande wa mashtaka umethibitisha kosa bila kuacha shaka dhidi ya washtakiwa wote nawatia hatiani kwa kosa la wizi wa kutumia dilaha kama walivyoshtakiwa.”

Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Gloria Mwenda, ambaye alidai  aliwashtaki wakosaji wa mara ya kwanza na akaomba wapewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa jamii.

Maoni