Mkakati utoaji huduma za afya kwa mfumo wa kadi waandaliwa

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inafanyia kazi mkakati mpya wa utoaji huduma za afya kwa mfumo wa kadi.
Amesema Serikali inaangalia namna ya kutumia vyanzo vya ndani vya mapato kukamilisha azma hiyo.
Samia amesema hayo leo Jumatano Oktoba 25,2017 alipozindua kongamano linalolenga kukuza maadili ya kitabibu na kitaaluma miongoni mwa wataalamu wa afya.
Akizungumzia kauli ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kuhusu wingi wa wagonjwa wenye msamaha wa matibabu, Samia amesema ili kukabiliana na ongezeko la gharama za matibabu kwa wananchi, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa muswada wa bima ya afya kwa wote.
Amesema muswada huo utamlazimu kila Mtanzania kuwa mwanachama wa bima ya afya.
"Tunaamini mfumo huu utamwondolea usumbufu mwananchi kutopata matibabu anapohitaji,” amesema.
Makamu wa Rais amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuwatambua wazee wasiojiweza wenye umri wa miaka 60 na zaidi katika kila halmashauri ili wapatiwe vitambulisho.

Maoni