Nani mbabe mechi ya 84, Simba na Yanga

MAHASIMU wa jadi katika soka la Tanzania, Simba na Yanga zinatarajia kukutana Jumamosi ijayo ama kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam au Uwanja wa Taifa.
Kama itachezwa Uwanja wa Uhuru itakuwa ni mara ya kwanza baada ya miaka 11.
Mara ya mwisho timu hizo kupambana kwenye uwanja huo ilikuwa ni Oktoba 29, 2006 kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu).
Timu hizo zilitoka suluhu bila kufungana. Mechi hiyo itakayochezwa Oktoba 28 ambayo Yanga itakuwa wenyeji itakuwa ni ya raundi ya nane ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea kutimua vumbi nchini.
Rekodi zinaonyesha kuwa baada ya mechi hiyo, timu hizo hazijawahi kucheza tena uwanja huo, kwani mechi iliyofuata Julai 8, 2007 ilichezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Ikumbukwe ilikuwa ni mechi ya Ligi Ndogo kutafutwa bingwa, kabla ya kuanza kwa mfumo mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulioanza kuchezwa mwezi Agosti na Septemba kama ilivyo nchi nyingi barani Ulaya.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwa dakika 120 baada ya timu hizo kuigia fainali katika mtindo wa mtoano, zilitoka sare ya bila kufungana na Simba kufanikiwa kutwaa ubingwa kwa mikwaju ya penalti 5-4.
Mechi ya kwanza Simba na Yanga kuchezwa kwenye uwanja mkuu wa Taifa ilikuwa ni Oktoba 26, 2008 iliyoisha kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Ben Mwalala dakika ya 15 ya mchezo.
Mechi ya 84
Itakuwa ni mechi ya 84 timu hizo kukutana kwa michezo ya ligi tu, tangu ilipoanzishwa mwaka 1965 wakati huo ikiitwa Ligi ya Taifa.
Mpaka sasa watani hao wameshapambana mara 83 kwenye mechi za Ligi Kuu peke yake.
Yanga bado vinara kwa Simba
Kati ya mara 83 ambazo timu hizo zimekutana, Yanga inaongoza kwa kuifunga Simba mara nyingi zaidi.
Yanga imeifunga Simba mara 31, huku Simba yenyewe ikiwa imeichapa Yanga mara 24 na kutoka sare mara 28.
Simba mbabe wa Yanga karne ya 21
Tangu kuanza kwa karne mpya ya 21, Simba imeifunga Yanga mara nyingi zaidi.
Kwa mujibu wa rekodi zilizopo ni kwamba, Simba imefunga Yanga mara 11 kuanzia mwaka 2000 ikiwa ni mwanzo wa karne ya 21.
Simba na Yanga zimecheza mara 33 kwenye Milenia, Yanga ikishinda mara saba na timu hizo zimetoka sare mara 15.
Kichuya kuweka rekodi ya Tambwe?
Winga wa Simba Shiza Kichuya, iwapo atafunga kwa upande wa Simba basi atakuwa akiifunga Yanga kwa mara ya tatu mfululizo na kujitengenezea rekodi kwenye mechi hizo za watani.
Alifunga goli Oktoba Mosi 2016, Simba ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga mechi ya kwanza msimu uliopita, huku akifunga bao mechi ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo, Februari 25 mwaka huu, Simba ikishinda mabao 2-1.
Straika wa Yanga, Amissi Tambwe ana rekodi ya kuifunga Simba mara tatu mfululizo.
Alifanya hivyo, Septemba 26, 2015, alipofunga goli moja, Yanga ikishinda mabao 2-0, lakini pia goli lingine alilifunga Februari 20 mwaka jana akifunga bao, Simba ikilala tena kwa mabao 2-0. Oktoba Mosi mwaka jana alifunga bao moja, timu hizo zikitoka sare bao 1-1, lakini alishindwa kuendeleza rekodi ya kufunga mfululizo, aliposhindwa kufanya hivyo, Yanga ilipolala mabao 2-1 Februari 25 mwaka huu, mechi ya mzunguko wa pili msimu uliopita.
Ajibu kufunga kwa mara ya kwanza?
Straika wa Yanga, Ibrahim Ajibu kama akifunga bao, ataweka rekodi ya kufunga goli kwa mara ya kwanza kwenye historia yake ya soka nchini.
Tangu apandishwe kikosi cha kwanza cha Simba mwaka 2013, hajawahi kuifungia Simba goli lolote kwenye mechi za watani.

Maoni