Rekodi 5 kali raundi ya 7 Ligi Kuu

RAUNDI ya saba ya Ligi Kuu Tanzania Bara imemalizika wiki hii.
Kama kawaida msimu huu, ligi imeendelea kuwa ngumu, huku kila timu ikijitahidi kupata ushindi, hali inayosababisha wakati mwingine kuwe na sare nyingi.
Raundi hii pia imetengeneza rekodi kadhaa ambazo zimewekwa na wachezaji, pamoja na timu zilizocheza.
Zifuatazo ni rekodi 10 zilizowekwa baada ya mechi za mwisho wa wiki hii.
1. Okwi kufunga mechi zote U/Uhuru
Straika wa Simba, Emmanuel Okwi amefunga tena goli kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuendeleza rekodi yake safi ya kufunga goli au magoli kila anapocheza kwenye uwanja huo.
Simba imecheza mechi nne kwenye uwanja huo na zote, Okwi ametupia.
Jumamosi alifunga bao moja, akiisaidia Simba kushinda mabao 4-0 dhidi ya Njombe Mji.
Mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Ruvu Shooting, Agosti 26 alipofunga magoli manne, Simba ikishinda mabao 7-0.
Mechi nyingine ilikuwa ni Septemba 17 alipofunga magoli mawili kwenye ushindi wa mabao 3-0 iliyoupata Simba dhidi ya Mwadui FC, huku Oktoba 15 akifunga bao la kusawazisha dakika za majeruhi dhidi ya Mtibwa Sugar na kusababisha sare ya bao 1-1.
Kwa sasa straika huyo Mganda amefikisha magoli manane, akiendelea kuongoza kwenye orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu.
2. Mbao kupata sare nne mfululizo nyumbani
Haijulikani kama ni mkosi au bahati mbaya kwa timu ya Mbao FC, kwani pamoja na kuonekana kuwa tishio kwenye Ligi Kuu hasa kwa timu kubwa, lakini imeendeleza rekodi ya kutoka sare mfululizo kwenye uwanja wake wa nyumbani, CCM Kirumba Mwanza.
Kwa mara nyingine tena, imetoka sare, lakini hii ni ya bila kufungana na Azam FC Jumamosi iliyopita.
Hii ni sare ya nne mfululizo kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Mbao mpaka sasa haijashinda hata mechi moja, ikicheza CCM Kirumba na mechi pekee iliyopata ushindi, ilikuwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar.
Simba ndiyo iliyoanza kuitua ‘gundu’ Mbao, kwani Septemba 21, zilitoka sare ya mabao 2-2 kwenye uwanja huo.
Baada ya hapo, Mbao ilicheza dhidi ya Prisons hapo hapo Kirumba, Septemba 30 na kulazimishwa sare ya bao 1-1.
Oktoba 13, Mbao iliendeleza mdudu wa sare ilipolazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mbeya City, kabla ya Jumamosi kukutana na sare ya nne mfululizo nyumbani ilipotoka sare ya bila kufungana dhidi ya Azam FC.
3. Mzamiru kufunga kwa mara ya kwanza
Kiungo wa Simba Mzamiru Yassin amefunga kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya raundi sita kupita.
Jumamosi iliyopita alifunga magoli mawili, Simba ikiibamiza Njombe Mji mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Uhuru.
Kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa wa kufunga magoli, alikuwa hajafanya hivyo kama ilivyokuwa kawaida yake msimu uliopita, huku kiwango chake pia kikionekana kushuka.
Msimu uliopita alikuwa ndiye kiungo wa kati aliyeongoza kufunga magoli mengi kwenye Ligi Kuu, kwani alipachika mabao manane.
4. Pluijm ana mkosi Nangwanda Sijaona
Kocha wa timu ya Singida United, Hans van der Pluijm aliendeleza rekodi yake mbaya kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, alipokanyaga tena na kuondoka bila ushindi.
Hii ni baada ya timu anayoifundisha, Singida United kutoka sare ya bila kufungana na wenyeji Ndanda FC.
Wakati akiifundisha Yanga, kocha huyo hajawahi kushinda kwenye uwanja huo.
Mara ya kwanza alikwenda kwenye uwanja huo akiwa na Yanga Mei 9, 2015 na timu yake kuondoka na kichapo cha bao 1-0 msimu wa 2014/15, lakini msimu uliofuata 2015/16 Yanga haikucheza mechi kwenye uwanja huo na badala yake ikautumia Uwanja wa Taifa kucheza mechi ya ugenini dhidi ya Ndanda Mei 14.
Hata hivyo, haikuwa dawa, kwani timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2, hivyo hata kama ingehesabika kuwa imechezeka Nangwanda Sijaona, bado Pluijm alishindwa kupata ushindi.
Msimu uliopita, Pluijm alikwenda tena Nangwanda Sijaona akiwa na Yanga na hakuweza kushinda, bali kupata sare ya bila kufunga mechi iliyochezwa Septemba 7 mwaka jana, kabla ya kuondoka na kujiunga na Singida United.
5. Mbao yashindwa kufunga kwa mara ya kwanza
Rekodi nyingine kwenye raundi ya saba ya Ligi Kuu ni timu ya Mbao FC kushinda kufunga goli lolote kwa mara ya kwanza.
Raundi zote sita zilizopita, timu hiyo imekuwa ikifunga goli au magoli kwenye mechi zake.
Sare ya bila kufungana dhidi ya Azam FC siku ya Jumamosi, imehitimisha rekodi yao hiyo safi ya kutupia kila ‘gemu’.
Kwenye mechi zake zilizopita, Mbao ilipata bao ugenini kwa kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, mechi ya pili ikipata bao licha ya kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Singida United na mechi ya tatu pia ilitupia goli moja, licha ya kupoteza mechi kwa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mechi yake ya nne, ilifunga magoli mawili ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Simba, ya tano ikifunga pia na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Prisons.
Mechi ya mwisho Mbao kupata goli, ilikuwa dhidi ya Mbeya City ikitoka sare ya mabao 2-2, kabla ya rekodi yake kuharibiwa kwa sare ya bila kufungana dhidi ya Azam.

Maoni