Shaaban Robert : Hazina ya lugha ya Kiswahili

Shaaban Robert alizaliwa tarehe 1 Januari 1909 katika kijiji cha Vibambani jirani na Machui ,
kilomita 10 kusini mwa mji wa Tanga.
Wazazi wake wote wawili walikuwa wa ukoo wa
Mganga wa kabila la Wayao, lakini hakujiita Myao kabisa, bali alikuwa mmojawapo wa wachache ambao daima walijiita Waswahili.
Hatujui sana habari za wazazi wake, lakini twajua kwamba jina la baba yake halikuwa Robert. Jina hili ama latokana na matamshi mabaya ya jina lake hasa, ama yawezekana ni jina alilopewa alipokuwa skuli Msimbazi . Inasemekana kuwa pengine alipewa na Mzungu mwenye asili ya Uingereza ambaye aliitwa Robert na aliwaomba wazazi wake wamtaje jina hilo. Kwa muda mfupi yeye mwenyewe aliandika jina lake ‘Roberts’, lakini baadaye aliacha kuliandika hivyo.
Alipata elimu yake katika shule ya Msimbazi,
jijini Dar-es-Salaam kati ya miaka 1922 na
1926 , akawa mtu wa pili katika wanafunzi kumi na mmoja waliofaulu mitihani yao na kupewa
shahada ya kutoka chuoni , yaani School Leaving Certificate.
Akaajiriwa na serikali ya kikoloni akawa karani katika idara ya forodha huko Pangani miaka 1926 – 1944 . Bila shaka kukaa kwake miaka mingi hivi katika mji wa kihistoria uliokuwa mahali pa utamaduni wa Waswahili tena mahali patulivu kulisaidia maendeleo yake Shaaban kama mwandishi wa Kiswahili.
Tangu mwaka 1944 hata 1946 alihamia ofisi nyingine ya Hifadhi ya Wanyama, baadaye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga (tokea mwaka
1952 hata 1960).
Alipandishwa cheo kuwa Grade III Higher Division mwaka 1929 , na katika mwaka wa 1944 akapandishwa tena kuwa Grade II Local Service.
Kwa ujumla Shaaban Robert aliandika vitabu
ishirini na mbili . Baadhi ya vitabu hivi ni: Adili na Nduguze , Kusadikika , Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad , Baada ya Miaka Hamsini, Utubora Mkulima na Maisha Yangu.
Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha za
Kichina , Kiingereza na Kirusi .
Mbali na maandiko yake alikuwa na athari kubwa katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili akiwa mjumbe wa kamati za East Africa Swahili Committee , East Africa Literature Bureau na
Tanganyika Languages Board . Alikuwa pia mwanachama wa Tanga Township Authority.
Alifariki dunia huko Tanga tarehe 22 Juni 1962 akazikwa Machui. Aliacha wake watatu na
watoto watano, ingawa aliwazaa kumi . Mke wa kwanza alikuwa Mdigo . Pia aliacha dada yake (wa baba mmoja) Mwana Saumu, na mama yake.
Alitunza kwa zawadi ya waandishi inayoitwa ‘Margaret Wrong Memorial Prize’; pia alikuwa ametunzwa nishani ya M.B.E.
Vitabu vyake
1.Maisha yangu
2.Kusadikika nchi iliyo angani
3.Kufikirika
4.Adili na nduguze
5.Masomo yenye adili
6.Utenzi wa Vita vya Uhuru
7.Wasifu wa Siti Binti Saad
8.Baada ya Miaka Hamsini
9.Utubora Mkulima

Maoni