WATANZANIA WANAOKAMATWA CHINA MADAWA WAFYEKWA.

Kufyekwa kwa kiwango hicho kulibainishwa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Kamishna Robert Boaz, katika mahojiano mahsusi na Nipashe mwishoni mwa wiki.
Alisema mafanikio hayo yametokana na jitihada za serikali kudhibiti mianya yote uingizaji na usafirishaji wa dawa hizo.
"Hivi karibuni nilikuwa China, niliuliza kwenye ubalozi wetu hali ya dawa za kulevya kwa Watanzania wanaokamatwa, wakaniambia kuna matukio manne kwa mwaka huu, na sasa tuko Oktoba, maana yake hali ni nzuri," alisema Kamishna Boaz.
"(Hii ni) Tofauti na kipindi cha nyuma matukio yalikuwa si chini ya 20 hadi 30 kwa mwaka Watanzania kukamatwa nchini humo kwa kusafirisha dawa za kulevya."
Alisema zipo mbinu nyingi zinazotumiwa na mamlaka kuziba mianya yote ya usafirishaji dawa hizo. DCI Boaz hakuwa tayari kuanika mbinu hizo, hata hivyo.
DCI Boaz alisema Tanzania siyo wazalishaji wa dawa hizo lakini zinatoka kwingine na zinapitishiwa nchini kwenda nchi za Ulaya, Marekani na China na kiasi kidogo ndiyo kinabaki kwenye matumizi ya ndani.
“Kutokana na udhibiti mkubwa nchini kwa sasa toka vita hii imeshika kasi, wafanyabiashara wengi hawapitishi dawa kwenye njia walizokuwa wanatumia," alisema, "haya ni mafanikio makubwa na tutaendelea kudhibiti kila mahali.
"Lengo ni kufikia sifuri, yaani Tanzania bila dawa za kulevya, na hili linawezekana iwapo kila mmoja atawajibika katika nafasi yake."
WANYONGWE
Kupungua kwa kwa kiasi kikubwa kwa matukio hayo kuna kuja miezi nane tangu Rais John Magufuli aseme serikali haitajishughulisha na Watanzania waliokamatwa ughaibuni na kuhukumiwa kunyongwa kutokana na kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
Akizungumza Ikulu, Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema orodha aliyonayo inaonyesha kuna nchi 17 zenye jumla ya Watanzania 663 waliokamatwa kwa kukutwa na madawa ya kulevya huku China ikiongoza kwa kuwa na wafungwa 268 kutoka nchini.
Rais Magufuli alisema Msumbiji kuna Watanzania 20 waliofungwa baada ya kukamatwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya, Nepal (wanne) na India (26).
Nchi nyingine, alitaja Rais Magufuli ni Uturuki (38), Ugiriki (25), Malaysia (16), Indonesia (mmoja) Comoro(watatu), Pakistan (watatu), Japan (60), Nigeria (91), Ghana (mmoja), Uingereza (24), Kenya (66), Misri (wawili) na Uganda (15).
Rais aliwataka mabalozi wa Tanzania walioko katika nchi mbalimbali kutojihusisha kwa vyovyote na wafungwa wa makosa ya madawa ya kulevya.
"Watanzania waliohukumiwa nje ya nchi kwa kujihusisha na dawa za kulevya, mabalozi msijihusishe nao... waacheni," Rais Magufuli alisema.
"Kama wamefungwa kifungo cha maisha, waacheni wafungwe, kama wamehukumiwa kunyongwa, wanyongwe tu. Tukichekacheka, taifa litaathirika na dawa za kulevya."
Rais Magufuli alituma 'salamu' hizo mara baada ya kuwaapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Dk. Anna Peter na mabalozi watatu.

Maoni