Barabara Yasababisha Nauli kupanda kutoka 4000 hadi 30,000/-

Gharama za usafiri hasa wa pikipiki kwenda na kurudi Ukwama kata ya Ukwama wilayani Makete mkoani Njombe imeongezeka kutoka shilingi 4000 kwenda na kurudi hadi kufikia shilingi 30,000

Hali hiyo imesababishwa na matengenezo ya barabara hiyo yanayoendelea hivi sasa kuanzia eneo la Ihobwela hadi Ukwama ambapo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha matengenezo ya barabara hiyo yamesimama kwa muda

Akizungumza katika kipindi cha Drive Home kinachorushwa na kituo cha redio Green FM Diwani wa kata ya Ukwama Mh. Augustino Tweve amesema mabasi ya abiria yaliyokuwa yakifanya safari zake hadi Ukwama yamesitisha safari kutokana na barabara hiyo kuwa mbaya kwa sasa

Amesema kwa sasa watumiaji wa barabara hiyo wanapata adha kubwa kutokana na mabasi ya abiria kusitisha huduma za usafiri, na nauli ya usafiri wa pikipiki kupanda huku akibainisha kuwa bado anaendelea kuhangaika kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri kuhakikisha barabara hiyo inafanyiwa matengenezo na mkandarasi ambaye yupo eneo la kazi

Kwa upande wake Mkandarasi wa Barabara hiyo Bw. Asajile Mbwilo amesema sababu zilizopelekea tatizo hilo ni mvua zinazoendelea kunyesha kuzuia shughuli zao kuendelea lakini mpaka sasa yupo eneo la kazi na mvua zikipungua matengenezo yataendelea

Amesema awali alikuwa akitegemea greda la halmashauri ambalo lilipata hitilafu na tayari ametafuta greda lingine ambalo limeshasambaza vifusi mpaka kijiji cha Utweve lakini mvua iliyonyesha ndiyo imezuia rola kushindilia barabara hiyo

Amewatoa hofu wananchi kuwa matengenezo hayo yatafanyika na barabara hiyo itakuwa nzuri na kuwataka pia itakapokamilika wananchi watoe pia pongezi kwa kazi nzuri badala ya kuishia kulaumu tu pale matengenezo yanapoendelea.

Maoni