NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ni

miongoni mwa wachezaji 30 walioteuliwa kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka Afrika.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pia limetaja orodha ya wachezaji 30 wengine kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka Anayecheza Afrika.
Washindi wa tuzo zote watatokana na kura za Makocha Wakuu nanWakurugenzi wa Ufundi wa vyama na mashirikisho ya Soka wanachama wa CAF pamoja na jopo la wataalamu kutoka kwenye vyombo vya habari mbalimbali Afrika.
Sherehe za tuzo zinatarajiwa kufanyika Alhamisi ya Januari 4 mwaka 2018 mjini Accra, Ghana.
Samatta anayechezea KRC Genk ya Ugelbiji, amewahi kuwa Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika mwaka juzi, wakati huo anachezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambaye aliiwezesha kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wachezaji wengine wa Afrika Mashariki walioingia katika kinyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika mwaka huu ni mshambuliaji Mkenya, Michael Olunga wa Girona ya Hispania na kipa Mganda, Denis Onyango wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Maoni