Nimekuja kuipa ubingwa Azam FC – Bernard Arthur


MSHAMBULIAJI mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Bernard Arthur, tayari amewasili nchini leo Jumapili alfajiri akitokea Ghana.

Mara baada tu ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl Julius Nyerere (JNIA), Arthur ameweka wazi kuwa amekuja kuisaidia timu hiyo kumaliza kwenye nafasi nzuri kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwemo kutwaa ubingwa.

“Malengo yangu ni kujiunga na kuendeleza niliyofanya nchini Ghana kwa kuyaleta hapa natarajia mambo mazuri kama kila kitu kitakwenda vizuri kama unavyojua mambo ya mpira wakati mwingine kuna kupanda na kushuka yote haya ni fomu si unajua namna ya kuipata fomu.

“Nitajitahidi kujiweka vizuri, nitjitahidi kufanya mazuri kwa klabu, na kufanya mazuri binafsi, kufunga mabao kadhaa kama sitofunga basi angalau kutoa pasi nzuri za mabao na kuisaidia klabu kuwa kwenye nafasi nzuri na kutwaa taji la ligi,” alisema Arthur.

Arthur alisema anasmhukuru Mwenyezi Mungu kwa kufanikiwa kujiunga na klabu bora ya Azam FC huku akidai hiyo ni njia sahihi ya kufikia malengo yake.

“Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kufika salama Tanzania na najisikia vizuri kujiunga na klabu hii ya ajabu yenye baadhi ya historia nzuri…Nimeijua Azam FC kupitia wachezaji wenu Yakubu (Mohammed), Razak (Abalora) ambao ni rafiki zangu mmojawapo nilicheza naye Razak wameniambia kuhusu klabu.

“Ofa ilipokuja sikujiuliza chochote kuhusu kujiunga nayo, nafikiri kujiunga na Azam FC ni jambo zuri kwangu na zuri kwa kipaji changu na maendeleo yangu na timu pia,” alisema.

Mshambuliaji huyo anayesifika kwa kushambulia kwa spidi, kupiga mashuti, kufunga mabao na kusumbua mabeki, amefanikiwa kufunga jumla ya mabao 11 kwenye msimu ulioisha wa Ligi Kuu Ghana (GPL), ambapo mbali na kuichezea Liberty pia amewahi kupita WAFA SC ambayo iliwahi kumpeleka kwa mkopo kwa vigogo wa Ivory Coast, Asec Mimosa.

Sapraizi nyingine inakuja

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed, aliyeambatana na mchezaji huyo akitokea Ghana alipokwenda kufanya usajili wake aliweka wazi kuwa huenda kabla ya kumalizika kwa wiki ijayo timu hiyo ikafanya maajabu mengine katika usajili wa dirisha dogo unaoendelea hivi sasa utakaomalizika Desemba 15 mwaka huu.

“Kwanza niseme tu kwamba binafsi naweza nikasema ni moja kati ya usajili ambao naimani nao, unajua wakati mwingine kwenye usajili mashabiki lazima waelewe hiki kitu kwenye usajili ni gambling (bahati nasibu), yaani unaweza ukasajili mtu anawika sana lakini akija anakuwa hafanikiwi ama unaweza ukasajili mtu wa kawaida sana halafu akija anafanikiwa.

“Sasa usajili wa Bernard Arthur ni moja kati ya usajili ambao mimi binafsi nauona kwamba unanipa matumaini kwa kile ambacho tulikuwa tunakitafuta, tunatafuta mtu ambaye ni mfungaji lakini ni zaidi ya mchezeshaji,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Pengine labda kabla ya wiki haijaisha hii inayoanza Jumatatu basi tutafanya maajabu mengine na tuombe Mungu na huenda sapraizi ikaja, sapraizi itakuja kuna watu walikuwa wanaona tulikuwa Ghana, Zambia Kitwe, tumerudi sasa tunarudi tena Zambia na huenda hili la Zambia safari hii wale wote ambao walikuwa wanasema tukawaambia tumemaliza twendeni tukacheze mpira.”

Maoni