Azam fc yashindwa kukaa kileleni



Raundi ya 11 ya ligi kuu soka Tanzania Bara imehitimishwa Jumatatu Hii kwa mchezo mkali kati ya Wanarambaramba Azam FC na Wanatamtam Mtibwa Sugar.

Mtanange huo umepigwa katika uwanja wa Azam Complex na kushuhudia timu zote mbili zikitoka na alama moja baada ya Sare ya bao 1-1.

Mchezo huo ulikuwa mkali kwa kila timu ikishuhudia kocha wa Azam FC Aristica Cioaba akikaa jukwaani kufuatia adhabu aliyopewa na Shirikisho la Soka nchini TFF kukaa nje ya uwanja kwa michezo mitatu.

Kipindi cha kwanza kilitawaliwa zaidi na wageni Mtibwa Sugar ambao mbali na kumiliki mpira kwa asilimia 53 lakini pia walipiga mipira mingi langoni mwa Azam FC.

Usumbufu wa Mtibwa. 

Mtibwa Sugar wakiwatumia Salumu Kihimbwa, Ally Makarani na Stamil Mbonde walilishambulia lango la Azam kama nyuki wakikosa nafasi 4 za kuwapa uongozi lakini uimara wa Razak Abalora uliwanyima nafasi hiyo.

Enock Atta Agyei. 

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, Azam FC walirekebisha Makosa yao na kuanza kucheza kwa umakini zaidi na utulivu tofauti na kipindi cha kwanza.

Dakika ya 56 Mpira ulioanzia kwa Frank Domayo ambaye naye bila kusubiri alimuangalia Mbaraka Yusuph Abeid ambaye naye akapiga V Pass iliyomkuta Mghana Enock Atta Agyei na kupiga kichwa na kuzama moja kwa moja wavuni.

Bao la Kelvin Sabato. 

Kelvin Kongwe Sabato 'Kiduku' aliyeingia kuchukua nafasi ya Salumu Kihimbwa Aliwasawazishia Mtibwa Sugar kwa faulo ya moja kwa moja katika dakika ya 75 ya mchezo huo.

Bao hilo linaweka historia adhimu kwani kabla ya mchezo huo nyavu za Azam FC wakicheza katika uwanja wao wa nyumbani zilikuwa hazijawahi kuguswa.

Bao hilo lilidumu hadi kipyenga cha mwamuzi Erick Onoka kutoka Arusha kilipopulizwa kuashiria kumalizika kwa dakika zote 90.

Matokeo hayo sasa yanawafanya Azam kufikisha alama 23 na kushindwa kuwaondoa Simba kileleni huku Mtibwa Sugar wao wakifikisha alama 18 na kuendelea kukalia nafasi ya nne ya msimamo wa ligi kuu soka Tanzania Bara. 

Raundi ya 12.

Ligi Kuu itasimama kwa takribani majuma mawili kupisha michuano inayosimamiwa na Baraza la vyama vya soka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati 'CECAFA Challenge Cup' inayoanza Disemba 3 hadi 17 nchini Kenya.

Maoni