SIMBA KUANZA NA WAWILI DIRISHA DOGO

KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amewaambia waajiri wake kwamba, kama watafanya mpango na kumwongezea mastraika wawili matata, ubingwa utakuwa mapema tu.
Kwa mujibu wa kigogo wa Simba, klabu hiyo ina mpango wa kuwatema Juma Luizio na Laudit Mavugo, ambapo Omog amependekeza kuongezewa silaha mbili ambazo zitashirikiana na Emmanuel Okwi na John Bocco.
Licha ya kigogo huyo kutokuweka wazi nchi ambazo washambuliaji hao watatoka, lakini amelihakikishia DIMBA kwamba, hautakuwa usajili wa masihara, kwani wanafahamu wanakabiliwa na michuano migumu ya Kombe la Shirikisho Afrika hapo mwakani, lakini pia wakiutaka ubingwa wa Ligi Kuu kwa kila namna.
“Yani kwa jinsi tulivyojipanga msimu huu hakuna shaka ubingwa tutautangaza mapema, nikuambie tu kwamba tayari kocha wetu amependekeza kuongezewa nguvu kwenye safu yake ya ushambuliaji na hilo linafanyiwa kazi.
“Kuna uwezekano mkubwa Juma Luizio na Laudit Mavugo wakatemwa kutokana na viwango vyao kushuka, ambapo nafasi zao zitajazwa na hao wawili, ambao Omog amependekeza watafutwe,” alisema.
Kigogo huyo alisema wanataka kasi ya upachikaji wa mabao iwe kubwa, ndiyo maana wanataka kuitengeneza vizuri safu yao ya ushambuliaji, huku akidai hakuna idara nyingine watakayoifanyia mabadiliko.
“Kama unavyoona idara yetu ya ulinzi na ile ya kiungo ipo imara sana, sasa hapo hatuwezi kugusa chochote, isipokuwa hii safu ya ushambuliaji, nadhani mashabiki wetu watapata raha sana msimu huu, kwani mipango ni mikubwa,” alisema.
Katika msimamo wa ligi, Simba wanaongoza wakiwa na pointi 19, sawa na Azam FC, timu hizo zikizidiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, huku Yanga wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 17.
Tangu msimu wa 2011/12 Simba walipotwaa ubingwa, hawajafanikiwa kufanya hivyo tena, kitendo kilichosababisha wasishiriki michuano ya Kimataifa na sasa wanataka kufanya kweli.

Maoni