ZOEZI LA UNYWAJI DAWA ZA KINGATIBA ZA MABUSHA NA MATENDE LAENDELEA KWA KASI SIMU 2000.

Zoezi la kutoa kingatiba ya dawa kwa ajili ya magonjwa yaliyosahaulika ya Matende na Mabusha leo limeingia siku ya pili ambapo vituo 136 vinaendelea kutoa huduma hiyo.
Vituo hivyo vyenye watoa huduma 273 vinatoa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali ya Mikusanyiko ya Wilaya ya Ubungo.
Maeneo hayo ni masokoni, vituo vya afya vya umma na binafsi, makanisani, misikitini, vituo vya mabasi na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu.
Kama ilivyo ada mtoa habari kutoka kitengo cha habari Manispaa ya Ubungo alitembele vituo viwili vinavyotoa huduma hiyo vilivyopo Kata ya Sinza eneo la kituo cha mabasi SIMU 2000 na kuzungumza na watoa huduma wa hapo.
Akizungumza mmoja wa watoa huduma hiyo anayefahamika kwa jina la Maua Hamisi Omari alisema zoezi linaendelea vizuri na wananchi wanajitahidi kufika kwa wingi na kuwaasa wote waliopo majumbani kwenda katika vituo vinavyotoa huduma hiyo ili kupata kingatiba na kuwahakikishia kuwa dawa hizo hazina madhara kwa watumiaji.
"Zoezi linaendelea vizuri, Jana pekee katika eneo la simu 2000 kituo cha hapa stendi ya mabasi na sokoni tumehudumia wananchi zaidi ya 130 kwa maana hiyo mwitikio ni mzuri na wananchi waendelee kuhamasishwa kuja kupata kingatiba" alisema Maua.
"Kuna taarifa zinaenea mitaani kuwa dawa hizi zina madhara kwa binadamu napenda kutumia fursa hii kusema habari hizi si za kweli na nawahakikishia kuwa dawa hizi ni sahihi kwa matumizi ya binadamu na mjitokeze kwa wingi kwani kinga ni bora kuliko tiba" alisema Maua.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO.
HALMASHAURI YA MANISPAA YA UBUNGO.

Maoni