Asilimia 98 la saba waingia sekondari

KATI ya wanafunzi 662,035 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu, 650,862 sawa na asilimia 98.31, wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza awamu ya kwanza mwaka 2018.

Miongoni mwa waliofaulu wanafunzi 11,173 sawa na asilimia 1.69 hawajapata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza, hivyo Halmashauri ambazo hazijachagua wanafunzi hao zikamilishe haraka miundombinu ya madarasa ili waanze masomo Januari 15, badala ya Januari 8, mwakani, ambayo wanaanza wa awamu ya kwanza.

Aidha, wanafunzi wote 1,912 wenye mahitaji maalumu waliofanya mtihani wa darasa la saba na kufaulu, wote wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari mbalimbali za serikali nchini.

Akitoa taarifa kwa umma mjini hapa jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Sulemani Jafo alisema wanafunzi hao waliofaulu na kupangiwa shule za sekondari mbalimbali ni miongoni mwa wanafunzi 662,035 sawa na asilimia 72.75 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka huu na wakafaulu.

Alisema idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwakani, imeongezeka kwa zaidi ya wanafunzi 124,209 sawa na asilimia 23.58 ya wanafunzi 526,653 waliofaulu mwaka 2017.

Kutokana na wanafunzi 11,173 ambao ni sawa na asilimia 1.69 ya wanafunzi waliofaulu ambao hawapata kujiunga nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza, Waziri Jafo aliziagiza Halmashauri ambazo hazijachagua wanafunzi hao zikamilishe haraka miundombinu ya madarasa ili kuwaingiza wanafunzi hao shuleni. “Nimeshatoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa hiyo kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwakani,” alisema Jafo.

Alizitaja halmashauri sita za mikoa ambazo zimeshindwa kuwachagua wanafunzi kutokana na uhaba wa miundombinu kuwa ni pamoja na Lindi wanafunzi 170, mbeya (3,092), Rukwa (4,091), Manyara (1,268), Katavi (976) na Simiyu (1,576), zikamilishe haraka miundombinu ya madarasa na kuwaingiza watoto shuleni.

Jafo alizitaja halmashauri 15 ambazo zimeshindwa kuwapangia wanafunzi wote waliofaulu kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwakani katika awamu kwanza kuwa ni pamoja na Lindi (170), Chunya (80), wilaya ya Mbeya 207, jiji Mbeya (1,227) na Mbarali (1,578). Nyingine ni Kalambo (166), Nkasi (1,318) na halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga (1,054), Manispaa Sumbawanga (1,554), Babati (581), Hanang (687), Mpanda (262), nsimbo (714), mji Bariadi (369) na Busega (1,207).

“Wanafunzi ambao hawakupata nafasi ya kuchaguliwa katika awamu ya kwanza, naelekeza tena kwa mara ya pili, kuwa mikoa ikamilishe ujenzi wa miundombinu ili wanafunzi waliobaki waweze kuchaguliwa katika awamu ya pili,” alisema. Alisema wakati wanafunzi waliopata nafasi ya kuchaguliwa katika awamu ya kwanza, wanatakiwa kuripoti shuleni Januari 8, mwakani, wanafunzi ambao watachaguliwa awamu ya pili wanatakiwa kuripoti shuleni Februari 15, mwakani.

“Lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba wanapata nafasi ya kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza,” alisema. Jafo aliwaasa wazee na walezi ambao watoto wao wamekosa nafasi katika awamu ya kwanza, kuwa waendelee kuwa wavumilifu wakati mikoa inajiandaa kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wote kuanza masomo ya kidato cha kwanza.

Aliwapongeza wanafunzi wote walipata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali nchini, walionesha juhudi na nidhamu binafsi walipokuwa shuleni kama nyenzo ya kufanya vizuri. Pia aliwashukuru walimu, walimu wakuu, kamati za shule, waratibu wa elimu kata, viongozi wa halmashauri na wadau wa elimu kwa kutoa ushirikiano katika kusimamia uendeshaji na utoaji wa elimu bora nchini.

“Nawaomba wanafunzi wote waliochaguliwa kutumia fursa hii vizuri katika kujifunza na kuachana na anasa au starehe ambao mwisho wa siku zitawafanya wasifanye vizuri katika mitihani yao ya kihitimu kidato cha nne,” alisema Jafo.

Aliwataka wanafunzi hao waripoti shuleni tarehe iliyopangwa, mwanafunzi atakayechelewa kuripoti wiki mbili baada ya shule kufunguliwa, nafasi yake atapangwa mwanafunzi mwingine. “Halmashauri na mikoa hakikisheni mnaandaa mazingira bora ya kuwapokea wanafunzi hao siku ya kuripoti, pia angependa kuwaona maafisa elimu wa mikoa na wilaya wote wakipita shuleni kuona hali ya mapokezi ya wanafunzi wote,” alisema

Maoni