JINSI YA KUMHUDUMIA MKE WAKO ALIYE MJAMZITO.

Baada ya jukumu la kibiolojia la baba kumalizika na kupelekea mama kuwa mjamzito, ni lazima pia mwanaume kuwajibika kama sehemu ya ujauzito huo.
Mama kuwa mjamzito siyo hali ya ugonjwa, ila ni mojawapo ya hali katika maisha ya binadamu iliyo na changamoto nyingi. Wanaume wengi hukumbwa na wasiwasi,hushangazwa na wakati mwingine wasijue la kufanya, pamoja na kujiuliza “Ni nini jukumu langu juu ya ujauzito huu?”, Ni jinsi gani ninaweza kumwonyesha mama aliyebeba mtoto wangu kuwa ninamjali?,
“Kwa kuwa nakaribia kuwa baba, maisha yatakuwaje huko mbeleni?”.Lakini hali kama hiyo inapojitokeza hatutakiwi kuwa na wasiwasi bali kuwa na mikakati mipya ambayo itawasaidia wakati wa ujauzito hadi pale mama atakapojifungua. Mikakati hiyo ni pamoja na maandalizi ya jinsi mtakavyoweza kumlea mwanafalia huyo mtarajiwa.
Wakati mwanamama atakuwa anakabiliana na jukumu hilo jipya, unahitajika kumwuliza ni kwa jinsi gani unaweza kumsaidia. Zifuatazo ni njia kumi ambazo waweza kumsaidia mwenzi wako katika kipindi chote cha ujauzito.

JIELIMISHE KUHUSU UJAUZITO
Soma na jifunze kuhusu ujauzito, pia jitahidi kuilewa vizuri hali anayopitia. Atajisikia sio mpweke na kuona kuwa kumbe jukumu hilo siyo lake pekee, bali lenu wote kwa kuwa unailewa hali hiyo ya ujauzito iliyo na changamoto nyingi. Elewa katika kipindi cha ujauzito unatakiwa uwe mfariji, sababu ni kuwa kuna mabadiliko makubwa ya homoni katika mwili wake ambayo wakati mwingine hupelekea kuwa na hasira, huzuni,wasiwasi, kulia kwa sababu ambayo hukutegemea , kichefuchefu na kutapika kwa siku nzima. Kila mara kuwa msikivu kwa kile anachotaka kufanya.

TILIA MAANANI YALE YANAYOMKABILI.
Ni kawaida yetu wanaume kuchukulia jambo kwa urahisi hata kama ni jambo lisilowezekana. Endapo mwenzi wako atalalamika kuhusu hali ngumu inayomkabili katika ujauzito, kumbuka ndivyo anavyojisikia kwa wakati huo, na usichukulie kwa mtazamo wako binafsi na kujaribu kukosoa. Ila inapotokea hivyo, inakuwa ni nafasi pekee kwako kumfariji, kumuuliza jinsi unavyoweza kumsaidia na kumsaidia kwa jinsi ambayo itampunguzia maudhi yatokanayo na ujauzito.

ONYESHA MAHABA.
Wanawake hufarijika sana unapowaonyesha kuwa, pamoja na hali ya ujauzito bado wanabaki kuwa warembo na wenye mvuto. Mueleze mke wako ni jinsi gani urembo wake haukutetereka pamoja na ujauzito ulibadilisha umbo lake. Ingawaje sio kila mwanamama mjamzito atapenda kujamiaana na mwenzi wake, lakini bado anapenda kuwa karibu na mwenzi wake, kwa hiyo hakikisha unabadilika kulingana na anavyojisikia kuhusu kujamiaana.

MFANYIE MASAJI.
Hususan katika awamu ya tatu ya ujauzito (third trimester), kina mama wajawazito hukumbwa na uchovu sana. Anakuwa amebeba uzito wa mtoto tumboni, hupatwa na maumivu ya viungo, mgongo pia maumivu ya misuli na mtoto hucheza sana na kumsababishia mama kukosa usingizi wakati mwingine. Kama baba, moja ya jambo la upendo la kumfanyia mama aliyebeba mtoto wako tumboni mwake, ni kumfanyia masaji ya mwili ili kumpunguzia uchovu na maumivu ya mwili kabla ya kulala. Mfanyie masaji miguu yake, unyayo, ambapo kutaongeza mzunguko wa damu na kumpunguzia uvimbe wa miguu ambao husababishwa na hali ya ujauzito. Pia masaji ya mgongo kumpunguzia maumivu ya mgongo.

Maoni