Mitambo ya Umeme ikarabatiwe ndani ya wakati- Dkt Kalemani

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaagiza wasimamizi wa mitambo ya kuzalisha Umeme nchini kuwa na utamaduni wa kufanya ukarabati wa mitambo kwa wakati ili kuepusha uharibifu mkubwa wa mitambo hiyo na hivyo kupelekea Serikali kuingia gharama ya kuagiza mitambo mipya ya umeme.
Dkt. Kalemani aliyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Njombe ambapo alikagua baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme inayotumia mafuta katika wilaya ya Tunduru, Namtumbo na Songea.
Aidha, Dkt. Kalemani aliwataka wasimamizi wa vituo vya kuzalisha umeme kuhakikisha kuwa wanakuwa na akiba ya vipuri vitakavyotumika pindi mitambo inapopata hitilafu ili kuepusha wananchi kukosa umeme kwa muda mrefu, “agizeni vipuri mapema, suala la mitambo mnalijua” alisisitiza.
Dkt.Kalemani aliongeza kuwa, Serikali itasimamisha uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta kutokana na kuwa na gharama kubwa, mara baada ya mradi mkubwa wa kusafirisha umeme wa kilovolti 220 wa Makambako-Songea utakapokamilika ambapo wateja wengi wataunganishwa na huduma ya umeme kutoka gridi ya taifa ifikapo Agosti 2018.
Akielezea uwezo wa mtambo wa kuzalisha umeme katika wilaya ya Tunduru, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma Florence Mwakasege alisema, kituo cha kuzalisha umeme cha Tunduru kilianzishwa mnamo mwaka 1992 kikiwa na mashine mbili zenye uwezo wa kuzalisha kilowati 350 kila moja.
Alisema kuwa, uwezo wa kituo hicho kwa sasa ni kuzalisha Megawati 1.35 ambapo mahitaji halisi ni Megawati 1.2, umeme unaotosheleza mahitaji ya wananchi wa mji huo kutokana na kuwa na watumiaji wachache wa nishati hiyo.
Aidha Mwakasege alisema kuwa, kwa kituo cha Namtumbo wateja 850 wameunganishwa ambapo kiasi cha kilowati 350 za umeme zinazalishwa katika kituo hicho. Alisema kiasi hicho cha umeme kinachozalishwa hakitumiki chote kutokana na wananchi kutokuwa na mwamko wa kuunganishiwa huduma ya umeme.

Chanzo : Wizara ya Nishati

Maoni