Mzee Akilimali Achimba Mkwara Yanga

Baada ya hapo jana wanachama wa klabu ya Yanga wa matawi yote Tanzania kutangaza kusudio la kuandika barua kwa uongozi ili umfute uanachama Katibu wa baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali, mwenyewe ameibuka na kudai hakuna mwenye ubavu wa kumuondoa Yanga.
Mzee Akilimali amekuwa mstari wa mbele kupinga mchakato wa mabadiliko ndani ya klabu ya Yanga kila mara akisisitiza kufuatawa kwa utaratibu.
Mwaka jana wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji alipotangaza kuikodi Yanga kwa miaka 10, Mzee Akilimali alipinga mchakato huo akidai Yanga haiwezi kukodishwa kama masufuria ya shughuli!
Sasa amesema kama atafutiwa uanachama wake, atakwenda hadi Ikulu kwa Rais Magufuli kufikisha malalamiko yake.
“Nimezuia mabadiliko yapi, mimi ni kati ya wale tuliotaka mabadiliko hata wengine hawajawa wanachama.
“Tatizo hawa wenzetu wanataka mambo ya haraka na ili mradi kuwaridhisha watu. Lazima tufuate utaratibu na hii ni lazima.
“Kama wanataka kuigawa klabu wanajidanganya na mimi na wazee wenzangu kamwe hatuwezi kukubali,” amesema.

Maoni