ZANZIBARI HEROES uso kwa uso na KENYA fainali jumapili hii.

Timu ya soka ya Taifa ya Zanzibar imewavua ubingwa wa michuano ya CECAFA, timu ya soka ya Taifa ya Uganda baada ya kuwachapa mabao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali.


Mchezo huo ambao umefanyika katika uwanja wa Moi mjini Kisumu nchini Kenya, umeshuhudia mchezo mkali ambapo Uganda wakicheza kandanda safi kwa dakika zote walishindwa kuhimili mikimiki ya Zanzibar ambao walicheza kwa nidhamu kubwa na kujituma muda wote.

Bao la Makame.

Zanzibar ndio walikuwa wa kwanza kugusa nyavu za Uganda ambapo, dakika ya 21 Ibrahim Hamad Ilika, alifanya jaribio zuri kwa kupiga shuti kali kwa guu la kulia,  lakini mlinda mlango Ismail Watenga akapangua na kuwa kona.

Kona hiyo ilienda kuchongwa na Adeyuni Saleh Ahmed ambaye Mpira wake ukamgusa Ibrahim Hamad naye kwa bila kuangalia akapiga mbele na kumkuta Abdul Aziz Makame aliyepiga kwa usahihi na kuandika bao la kuongoza kwa Zanzibar.

Bao la Uganda.

Bao hilo halikudumu sana kwani dakika ya 29 Uganda wakasawazisha baada ya walinzi wa Zanzibar kufanya uzembe na kumruhusu Mutyaba Muzamir kupiga krosi iliyomkuta Derick Nsibambi na kuandika bao la kusawazisha.

Mpaka timu zinakwenda mapumziko Licha ya mabao kuwa 1-1 lakini Uganda walionekana wakiwa na muunganiko mzuri zaidi, wakimiliki mpira kwa asilimia 62 huku wakipiga mashuti matano kuelekea langoni mwa wapinzani wao, tofauti na yale manne ya Zanzibar Heroes.

Bao la MO Banka.

Nsubuga Joseph katika dakika ya 55 akijaribu kumzuia Ibrahim Hamad kufuatia Zanzibar kuanzisha shambulio la kushtukiza anapewa kadi nyekundu na Mwamuzi akaamuru penati.

Penati ilipigwa na Mohamed Issa 'MO Banka' na kumchambua umaridadi mlinda mlango Ismail Watenga na kuandika bao la pili, lililowapa uongozi kwa mara nyingine.

Bao hilo lilidumu hadi kipyenga cha mwamuzi kutoka Rwanda kilipopulizwa na rasmi Uganda kuvuliwa ubingwa ambao waliupata mwaka 2015 nchini Ethiopia.

Kwa mantiki hiyo sasa Zanzibar watacheza mchezo wa fainali siku ya jumapili dhidi ya wenyeji Kenya katika michuano hiyo inayosimamiwa na Baraza la vyama vya soka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati 'CECAFA'.

Walioanza upande wa Uganda: Ismail Watenga (GK); Nico Wakiro Wadada, Shafiq Bakaki, Bernard Muwanga (Captain), Aggrey Madoi; Allan Kyambadde, Muzamiru Mutyaba, Tadeo Lwanga; Derrick Nsibambi, Hood Kaweesa, Militon Karisa

Akiba: Tom Ikaara (GK), Benjamin Ochan (GK), Joseph Nsubuga, Ibrahim Sadam Juma, Nelson Senkatuka, Allan Kateregga, Daniel Isiagi, Tom Masiko, Paul.

Walioanza Zanzibar: Mohammed Abrahman (Wawesha) 18, Ibrahim Mohamed Said (Sangula) 15, Adeyum Ahmed Seif 20, Abdulla Salum Kheri (Sebo) 13, Issa Haidar Dau (Mwalala) 8, Abdul azizi Makame Hassan (Abui) 21, Mohamed Issa Juma (Banka) 10, Mudathir Yahya Abass 4, Ibrahim Hamad Ahmada “Hilika” 17, Feisal Salum Abdallah (Fei Toto) 3, Suleiman Kassim Suleiman “Seleembe” 7 (nahodha).

Akiba: Ahmed Ali Suleiman (Salula) 1, Nassor Mrisho Salim 30, Mohd Othman Mmanga 6, Ibrahim Abdallah Hamad 2, Abdullah Haji Shaibu (Ninja) 5, Seif Abdallah Rashid (Karihe) 12, Hamad Mshamata Makame 9, Khamis Mussa Makame (Rais) 28, Abdul swamad Kassim Ali (Hasgut) 22.

Maoni