CCM HAIWEZI KUONDOKA MADARAKANI LEO WALA KESHO, VYAMA VINGINE VINAPOTEZA MUDA TU: KHERI JAMES

Na Mathias Canal, Arusha 

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa umesema kuwa katika kipindi ambacho vyama vya upinzani havitakiwi kufikiria kabisa kuhusu kushika dola ni pamoja na kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kutokana na utendaji wake uliotukuka kwa maslahi ya wananchi..

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Umoja huo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Taifa Ndg Kheri Denice James wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji na Kata ya Longido kwenye mkutano wa hadhara akimnadi mgombea Ubunge kwa tiketi ya CCM Jimbo la Longido Dkt Steven Kiruswa.

Kheri Alisema kuwa wananchi wa Longido wamepata mgombea mzuri, msomi na mwenye hofu ya Mungu atakayeweza kuwasilisha shida zao na kupatiwa utatuzi tofauti na wagombea wengine wa vyama bubu.

Alisisitiza kuwa Vijana na wananchi wa Longido kwa ujumla wao wanapaswa kuwa na muwakilishi mzuri bungeni ambaye ataweza kumudu kasi ya Rais Magufuli katika mtazamo wake wa kutatua na kuzipatia ufumbuzi kero za wananchi.

Kheri aliongeza kuwa vyama vya upinzani nchini vipo katika wakati mgumu kwani vimekuwa na agenda ya kutegemea serikali ikosee ndipo viseme jambo ambalo kwa sasa Rais Magufuli anasimamia vyema ilani ya uchaguzi na kutatua shida za wananchi hivyo upinzani kukosa muelekeo.

Wakati huo huo Mwenyekiti Kheri ametoa pole kwa wakazi wa Kata ya Oloirien Wilaya ya Arusha Mjini kwa kumpoteza kijana mahiri na mchapakazi Ndg Justine Kasanga aliyepoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount Meru.

Alitoa pole kwa familia kutokana na kumpoteza kijana wao mpendwa lakini pia Chama Cha Mapinduzi ambapo amewataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

MWISHO

Maoni