HIZI NDIO MBINU ZA LWANDAMINA LEO DHIDI YA AZAM FC


Ni moja ya mechi nzuri ambayo wapenzi wa soka nchini wamebahatika kuishuhudia jioni ya leo. Timu zote yaani Yanga SC washindi na Azam FC zimeonesha ubora wao kwanini wapo nafasi za juu katika msimamo wa ligi.

Ni takribani misimu mitano sasa mechi ya wawili hawa imekuwa na ushindani mkubwa ikitanguliwa na mechi ya watani wa jadi Yanga SC na Simba.

Azam FC waliingia uwanjani wakiwa wamejidhatiti kuondoka na alama tatu dhidi ya bingwa mtetezi Yanga SC ili kujiweka vyema katika mbio zao za kuusaka ubingwa wa ligi pia kulinda heshima yao ya kutopoteza mechi hata moja toka ligi ianze mwaka jana . Kabla ya mechi ya leo Azam walicheza mechi 14 bila kupoteza zilizowaweza kukusanya alama 30 wakitanguliwa alama mbili tu na Simba SC kileleni wenye alama 32.

Dakika ya tatu ya mchezo Azam FC waliweza kutimiza lengo la kupata goli la mapema ili kuwachanganya Yanga SC wakitumia mfumo wa 3-5-2 uliowawezesha Himidi Mao Mkami na Bruce Kangwa kupanda juu kwenye wings na kuipa shida Yanga SC dakika za awali ambayo ilikuwa ikitumia mfumo wa 4-3-3.

Goli la Shaaban Chilunda ikiwa kazi nzuri ya Kangwa aliyemshinda nguvu na maarifa Hassan Kessy liliwatanguliza mbele Azam FC lakini ndilo ambalo liliwaponza.

Azam walianza kujiamini na kucheza ‘ open game ‘wakipunguza pressure langoni kwa Yanga ambao baada ya goli hilo walibadili approach zao za kujilinda na kushambulia.

Lwandamina na wasaidizi wake licha ya kuonekana timu yao imezidiwa wing ya kulia, waliamua kuimarisha eneo la kiungo ili kuja na mpango mbadala katika kushambulia na kujilinda.

Rafael Daudi aliyepangwa kama winga wa kulia alipewa jukumu la kuendesha timu kati akimpa back up Juma Makapu ambaye mara nyingi si mzuri kupandisha timu juu na tayari Azam FC walionesha kuukata muunganiko wao na Papy Tshishimbi.

Mara nyingi kwenye 4-3-3 timu lazima iwe na viungo washambuliaji wawili wenye uwezo mzuri kuchezesha timu, kufunga pia kubadili mchezo . Kwa mchezo wa leo hili lilikuwa jukumu la Ibrahim Ajibu na Emanuel Martin lakini walinzi na viungo wa Azam waliweza kummudu Emanuel Martin na kujikuta timu inakosa mtu wa pili kumsaidia Ajibu na ndipo Rafael Daudi alipoanza kuonesha makali yake kulikamata jukumu hili ili umbo la timu lisipotee.

Azam walijitoa mchezo licha yakuwa na uwezo wa kumiliki mpira na kuisumbua vyema ngome ya Yanga, lakini walishindwa kuweka mpira chini na kujikuta mara nyingi wakitaka kutumia mipira mirefu kitu ambacho Yanga waliking’amua na pia uwezo wa kipa wao Rostand kuicheza mipira ya juu uliwasaidia.

Umiliki wa Yanga kwenye kiungo baada ya tactical set up ya Makapu, Tshishimbi, Rafael Daudi na Ajibu iliwafanya Yanga kuwa na uwezo mzuri kujenga mashambulizi ya upande .

Kabla ya kufunga goli la pili Yanga SC lililotiwa nyavuni na Gadiel Michael kwa mkwaju mkali, Gadiel mlinzi wa kushoto wa Yanga alipanda juu mara tatu akiweza kumgeuza Himidi Mao lakini bado Azam hawakuwa makini kumzuia kupanda wakimlinda zaidi Chirwa na Ibrahim Ajibu.

Pasi ya Tshishimbi kwa Gadiel Michael ambaye aliachia shuti kali umbali wa mita 29 na kutinga nyavuni ulikuwa uzembe kwa walinzi wa Azam waliomruhusu beki huyo kupanda mara ya nne akiwa huru wakijiamini sana na ulinzi wao.

Lakini pia golikipa wa Azam FC hakuwa katika kiwango chake ambacho wengi tumekizoea. Magoli yote mawili ya Yanga yalionesha udhaifu wake . Goli la kwanza la Chirwa kusawazisha ni kukosa umakini akajikuta analamwa chenga na Chirwa kutikisa nyavu. Goli la pili licha ya walinzi wake kushindwa kumfanyia marking Gadiel lakini alitoka goli bila yakuwa na hesabu nzuri ya kupunguza goli lake hali iliyompa nafasi Gadiel kumtazama toka mbali na kutikisa nyavu.

Ukiachilia mbali mbinu za bechi la ufundi na wachezaji takribani wote kujituma vyema kusaka ushindi mbele ya Azam , Yanga imeonesha bado ina uwezo wa kuulinda ubingwa wake endapo kujituma kwa wachezaji na viongozi wao kuwajali wachezaji katika masilahi na shida zao.

Maoni

  1. Chapisho hili limeondolewa na msimamizi wa blogu.

    JibuFuta

Chapisha Maoni