MD KAYOMBO AKABIDHIWA JENGO LENYE MADARASA MAWILI YA KISASA SHULE YA SEKONDARI URAFIKI

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo amekabidhiwa jengo la kisasa lenye Madarasa mawili katika shule ya Sekondari Urafiki Kata ya Ubungo Jijini Dar es Salaam.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 11/01/2018 katika viwanja vya shule ya Sekondari urafiki na Kampuni ya Tanzania steel pipes Ltd  mbele ya Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare Makori kwa Mkurugenzi Ndg Kayombo tayari kwa matumizi.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ndg John Lipesi Kayombo ambaye ndiye aliomba msaada wa Madarasa hayo mawili ya kisasa wakati anamkaribisha mgeni rasmi  Mhe .Kisare Makori alisema:

"Wakati nimeteuliwa kuwa Mkurugenzi nilifanya ziara katika shule hii ya sekondari urafiki nikakuta jengo lenye madarasa matano yote yakiwa chakavu hayafai kabisa kutumiwa na wanafunzi ndipo nikaagiza yabomolewe mara moja" alisema Kayombo.

"Kwa neema ya Mungu tukakutana na watu hao wa kampuni ya Tanzania Steel Pipes Ltd tukawaomba wakakubali kutujengea madarasa haya mawili ambayo ni imara na ya kisasa ambayo hayapo popote pale zaidi ya Ubungo" alisema Kayombo.

"Mkuu wangu wa wilaya naomba nikuhakikishie tutayatunza madarasa hayo na ile sehemu unayoiona ipo wazi tayari nimeshatenga fedha ya kujenga vyumba vitatu vya madarasa ili kukamilisha vyumba vitano vya madarasa" alisema Kayombo na kuendelea.

"Ili kuweka mazingira mazuri ya watoto wetu ya kufundishia na kujifunzia na hii yote ni kuhakikisha tunatekeleza ilani ya chama cha Mapinzi (CCM) ambacho ndicho chama Dola." Alisema Kayombo.

Pia Mhe. Kisare Makori baada ya kupokea Madarasa hayo amemshukuru mkurugenzi wa Kampuni  ya Tanzania Steel Pipes ndg Elly Bohela kwa msaada huo wa kizalendo.

Na akasisitiza makampuni mengine yaige mfano huo kwa kuwa kampuni hiyo ni mlipaji kodi mzuri na bado wameweza kutujengea madarasa imara ya kisasa tunawashukuru sana.

Aidha Kayombo amemuagiza kaimu mkuu wa idara ya Elimu Bi Neema Maghembe kuhakikisha mwl. Mkuu wa shule hiyo ya Sekondari kushirikiana na walimu wote katika shule hiyo kuyatunza madarasa hayo yaweze kudumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya vijana wetu.

Wadau tunawakaribisha Ubungo kwa pamoja tuijenge Ubungo

Imetolewa na :
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.

Maoni