Azam fc kuwakosa watano dhidi ya Ndanda.

Benchi la ufundi la timu ya soka ya Azam ‘Wanarambaramba’ limewahakikishia ushindi wapenzi wa timu hiyo licha ya kuwakosa wachezaji watano wa kikosi cha kwanza kuelekea mchezo wao wa ligi dhidi ya Ndanda FC ‘Wanakuchele’.

Azam itamkosa nahodha wake Himid Mao Mkami ambaye ni majeruhi, huku Waziri Junior, Joseph Kimwaga na Joseph Mahundi wakiendelea kuuguza majeraha yao wakati kiungo Abubakar Salumu ‘Sure Boy’ yeye atakosa mchezo huo kutokana na kuoneshwa kadi nyekundu katika mchezo uliopita dhidi ya Dar Young Africans.

Afisa habari wa Azam, Jaffary Idd Maganga amesema hawatatetereka kutokana na kuwakosa wachezaji hao kwani kikosi chao ni kipana na kila mchezaji anaweza kucheza hata wanapokosekana wengine.

“Tunashukuru Mungu kwamba tunakikosi kipana, kwa maana kwamba wachezaji wote wana uwezo na kila mmoja ana nafasi ya kucheza na mwalimu alikuwa ana wapa nafasi wote, hii ndio advantage kwani mmoja akiumia basi replacement inakuwepo kwa haraka,” Amesema.

Ndanda ni timu nzuri.

Katika hatua nyingine Maganga amesema mchezo wao dhidi ya Ndanda utakuwa mgumu licha ya kucheza katika uwanja wao wa nyumbani, kwani wanaijua timu wanayoenda kukutana nayo na namna walivyowagumu kufungika.

Mchezo uliopita baina ya timu hizo uliofanyika mjini Mtwara, Azam waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Yahaya Mohamed ambaye kwa sasa hayupo kikosini.

Mchezo huo utafanyika katika uwanja wa Azam Complex kuanzia majira ya saa moja kamili jioni, siku ya Jumamosi ya januari 3 mwaka huu.

Mechi nyingine za jumamosi.

Lipuli v Yanga – Samora, Iringa.

Stand United v Mtibwa – CCM Kambarage, Shinyanga.

Tanzania Prisons v Njombe Mji – Sokoine, Mbeya.

Majimaji v Mbeya City – Majimaji, Ruvuma.

Maoni