AZAM FC YAIPIGA KMC 3-1 YATINGA ROBO FAINAL ASFC

Mashariki na Kati, Azam FC, imetinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuichapa KMC mabao 3-1, mchezo uliochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Iliwachukua dakika 26 tu Azam FC kuweza kupata mabao yote matatu yaliyoipa ushindi, alianza kiungo Frank Domayo dakika ya kwanza akifunga bao la uongozi kwa shuti zuri akimalizia pasi Joseph Mahundi aliyepenyezewa mpira na Yahya Zayd,

Dakika tano baadaye mshambuliaji Mbaraka Yusuph, aliyekuwa kwenye kiwango kizuri aliipatia Azam FC bao la pili kwa shuti la ufundi akitumia vema pasi ya Zayd.

Zayd ambaye alipika bao la pili, aliweza kuhitimisha ushindi huo baada ya kuipatia bao la tatu Azam FC akimalizia pasi safi ya kiungo Domayo.

KMC ilijitutumua na kujipatia bao la kufutia machozi kupitia kwa Mohamed Hassan, aliyepiga kichwa na kufanya mchezo huo kwenda mapumziko kwa Azam FC kuongoza kwa mabao 3-1.

Kipindi cha pili Azam FC ilijitahidi kulinda ushindi ilioupata kipindi cha kwanza, ambapo KMC ilionekana kutawala mchezo lakini ilishindwa kufurukuta mbele ya safu ya ulinzi ya matajiri hao chini ya Nahodha Msaidizi, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, David Mwantika na Bruce Kangwa.

Kwa matokeo hayo, Azam FC hivi sasa inasubiria kupangiwa mpinzani wake kwenye hatua ya robo fainali na waandaji wa michuano hiyo, itakayofanyika wiki ijayo mara baada ya mechi zote za hatua ya 16 bora kukamilika.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika leo Jumapili kabla ya kuanza maandalizi ya kuikabili Singida United katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi ijayo saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, David Mwantika, Bruce Kangwa, Yakbu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue/Salmin Hoza dk 72, Salum Abubakar, Frank Domayo, Yahya Zayd, Mbaraka Yusuph/Shaaban Idd dk 79, Joseph Mahundi.

Maoni