BARAZA LA HABARI LIMEAMURU KUFUNGIWA KITUO CHA RADIO.

Baraza la habari nchini Rwanda limeamuru kituo kimoja cha redio kinachomilikiwa na raia wa Marekani kufungiwa matangazo kwa muda wa miezi mitatu, baada ya redio hiyo ya Kikristo kurusha mahubiri yanayowadhalilisha wanawake. Tarehe 29 mwezi Januari, kituo hicho kijulikanacho kama Amazing Grace FM kilirusha mahubiri ya mchungaji wa mjini Kigali, Nicolas Niyibikora, ambamo alisema wanawake ni watu hatari, waovu na wanaokwenda kinyume na mipango ya Mungu.

Mahubiri yake hayo yalizusha mjadala mkali miongoni mwa makundi ya wanawake, ambayo yalipeleka malalamiko katika Baraza la Habari la Rwanda linaloratibu vyombo vya habari nchini humo. Mkuu wa kamati ya baraza hilo Edmund Kagire alisema hapo jana kuwa mahubiri ya Niyibikora yanawadhalilisha sana wanawake, na kumtaka mchungaji huyo kuomba radhi hadharani. Kituo hicho kinamilikiwa na mwinjilisti wa kimarekani Gregg Schoof, ambaye tayari alikwishaonywa mara kadhaa kuhusu kurusha vipindi vyenye maudhui ya uchochezi.

Maoni