HUYU NDIE DENNIS OLIECH MCHEZAJI MWENYE HISTORIA. Mjue zaidi

DENNIS OLIECH:
WAMETOKEA wanasoka wengi Kenya ambao waling’ara kwenye Challenge, lakini kama ilivyo kwa wachezaji wa Tanzania unahitajika utulivu wa hali ya juu, ili kumtaja mmoja ambaye daima anastahili kukumbukwa katika historia ya michuano hiyo.

Mfungaji wa bao la tatu na la ushindi katika dakika ya 72 ya fainali ya Kombe la Challenge Desemba 14, mwaka 2002 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Tanzania Bara ikilala 3-2 na kupoteza matumaini ya kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu.

Nani zaidi ya Dennis Oliech. Na kwa nini asahaulike mtu huyo siyo tu kwa kuwakomoa wenyeji na kuwapokonya tonge mdomoni, bali soka yake iliyomuuza Ulaya baadaye.

Siku hiyo, Emmanuel Gabriel alitangulia kuifungia Bara dakika ya 28, kabla ya Paul Oyuga kusawazisha dakika ya 30 na Mecky Mexime kufunga la pili kwa penalti dakika ya 59 na John Barasa kuisawazishia Harambee Stars dakika ya 70 na Oliech kupiga la ushindi dakika ya 72.

Oliech alikuwa mfungaji bora katika fainali hizo kutokana na mabao yake matano, akiwa ana umri wa miaka 17 tu wakati huo.

Oliech alizaliwa Februari 2, mwaka 1985, baada ya kung’ara kwenye fainali hizo, mwaka 2003 alinunuliwa na Al-Arabi ya Qatar hadi mwaka 2005, aliposaini mkataba wa miaka minne na FC Nantes ya Ufaransa na kuanza safari yake kuogelea kwenye bwala la fedha Ulaya na sasa anachezea Auxerre.

Aliiwezesha Kenya kukata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2004 na alicheza vizuri kwenye fainali hizo nchini Tunisia na mwaka huo huo akatabiriwa kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari baadaye duniani, akiwekwa katika orodha moja na Wayne Rooney wa Manchester United. Oliech kwa sasa ameipa kisogo michuano ya Challenge, ingawa bado anaichezea Harambee Stars katika michuano mikubwa, ila Challenge ndio iliyomtoa.

Maoni