HUYU NDIYE MCHEZAJI ALIYECHEZEA ZAMBIA MECHI NYINGI ZAIDI.

KALUSHA BWALYA:
SAHAU kuhusu Zambia iliyochukua Kombe a Challenge mwaka 2006, wakati huo imekwishajitoa katika nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na kuingia nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA).

Zambia iliyotikisa katika soka ya Afrika Mashariki na kati ni ile iliyokuwa ikiitwa KK Eleven kuanzia miaka ya 1970 hadi 1990 mwanzoni, kabla ya ajali ya ndege iliyoua nyota wa kikosi hicho pwani ya Gabon mwaka 1993.

Kalusha Bwalya alikuwa katika orodha ya wachezaji waliotakiwa kuingia kwenye ndege iliyopata ajali, lakini bahati nzuri kwake alisema atatokea kwenye klabu yake moja kwa moja Ulaya kwenda Tunisia, hivyo akanusurika.

Katika historia yake ya ushiriki wa Challenge, KK Eleven ilibeba taji hilo mwaka 1984 na 1991 ambao, Kalusha Bwalya aliungana na Majid Musisi katika ufungaji bora, kila mmoja akifunga mabao yake matatu.

Challenge ya mwisho kwa Bwalya ilikuwa mwaka 1992 mjini Mwanza, alipoiongoza Zambia hadi Nusu Fainali ilipotolewa na Uganda kwa penalti 4-2, Uwanja wa CCM Kirumba kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.

Huwezi kuizungumzia historia ya Challenge bila ya kumtaja Bwalya, aliyezaliwa Agosti 16, mwaka 1963 mjini Mufulira, kwani enzi zake alikuwa mkali haswa.

Huyo ni mchezaji aliyeichezea Zambia mechi nyingi zaidi na kuifungia mabao mengi zaidi pia kuliko mchezaji yoyote hadi sasa. Ndiye mchezaji babu kubwa zaidi kuwahi kutokea katika ardhi ya Zambia. Unamzungumzia Mwanasoka Bora wa Afrika mwaka 1988, ambaye mwaka 1996 aliingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, ambayo ilichukuliwa na Mwafrika mwenzake, George Weah.

Maoni