Ishu ya Okwi kuwekewa ulinzi hii hapa

Emmanuel Okwi, ameomba waamuzi wamlinde ili aweze kufikia malengo yake kwani msimu huu anataka kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara timu yake ya Simba.

Okwi, raia wa Uganda, anaongoza kwa ufungaji katika Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 13, huku Simba ikiwa inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 41, baada ya kucheza mechi 17, ikibakiwa na mechi 13 kabla ya kumalizika kwa msimu huu.

Okwi ameomba ulinzi huo baada ya hivi karibuni kuchezewa vibaya na beki wa Ruvu Shooting, Mau Bofu hali iliyomfanya azimie uwanjani kwa dakika kadhaa kabla ya kupatiwa huduma ya kwanza na kurudi kwenye hali yake ya kawaida, lakini alishindwa kuendelea na mchezo huo ambao Simba ilishinda kwa mabao 3-0.

Akizungumzia kitu kinachomkera anapokuwa uwanjani kutimiza majukumu yake, Okwi amesema: “Kitu kinachonikera ni watu wanavyopania wenzao bila ya kumfikiria mwenzake atakuwa kwenye hali gani, kwa sababu tunapokuwa uwanjani wote tunafanya kazi na kazi yetu ni mpira.

“Familia zetu wote zinatuangalia kwa sababu tunacheza mpira na hela tunapata kwa ajili ya mpira, siyo vizuri kumpania mwenzio, marefa wanatakiwa wawe makini sana ili hali hii ikomeshwe.

“Binafsi nahitaji kuisaidia timu yangu kuchukua ubingwa msimu huu, sasa sitaki nishindwe kutimiza malengo yangu hayo kutokana na kuwa majeruhi kwa kufanyiwa faulo za makusudi.”

Maoni