JUHUDI ZA MKURUGENZI KAYOMBO ZAMUHAMASISHA MTENDAJI KUKARABATI OFISI YA KATA



Jumatatu 19 February 2018.

Ubungo, Dar es Salaam.

Mtendaji wa Kata ya Ubungo Ndg. Isihaka Waziri kwa kuona juhudi zinazofanywa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg. John Lipesi Kayombo za kutafuta wadau wa kuchangia shughili za maendeleo, ameendeleza ukarabati wa jengo la ofisi hiyo kwa fedha za michango kutoka kwa wadau mbalimbali wanaoishi katika Kata hiyo.

Ukarabati huo unahusisha kupiga rangi nje na ndani ya jengo hilo, kuweka tiles (vigae) na kuweka nyavu katika madirisha.


Jengo hilo lilitengenewa fedha kiasi cha shillingi Millioni 16 ambazo zilipatikana kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani ambazo zilitumika kupandisha ukuta, kufunga linta pamoja na kubadilisha paa, kwa mujibu wa BOQ (Bill Of Quantity) ambapo kazi zote hizo zilishakamilika.

Akizungumza wakati wa mahojiano na mtandao huu Ndg. Isihaka Waziri alimshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg. John Lipesi Kayombo kwa kumuamini na kuendelea kumuunga mkono katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika Kata ya Ubungo, jambo linalomfanya kuendelea kujituma zaidi.

Pia alimpongeza Mkurugenzi Kayombo kwa kazi nzuri anayoifanya na kuhakikisha Manispaa ya Ubungo inapiga hatua kimaendeleo.

"Nampongeza sana Mkurugenzi Kayombo, amekuwa kiongozi wa mfano kwa kutafuta wadau mbalimbali wa kuchangia maendeleo, nami kupitia mfano wake nimetafuta wadau kwa ajili ya kumalizia ukarabati wa jengo la ofisi yetu" alisema Waziri.

" Pia nampongeza Mkurugenzi Kayombo kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha Manispaa inasonga mbele na kuwa Manispaa ya mfano" alisema Waziri.

Sambamba na hayo Ndg. Waziri aliwashukuru wadau wote waliojitokeza kuchangia ukarabati huo na kutoa wito kwa wadau wengine waendelee kuchangia ili Kata ya Ubungo isonge mbele kimaaendeleo.

Imetolewa na
Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo

Maoni