KIZAAZAA CHAIBUKA KWENYE MKUTANO WA KIJIJI IHANGA, CHANZO FEDHA ZA CHOO


Wananchi wa kijiji cha Ihanga kata ya Ukwama wilayani Makete mkoani Njombe wamelaani vikali kitendo cha kamati ya kijiji hicho kutumia fedha za ujenzi wa choo cha wanafunzi katika shule ya msingi Ihanga Kwa shughuli zingine tofauti hali iliyopelekea kusimama kwa ujenzi wa choo hicho.

Hayo yamejitokeza hapo jana February 7, 2017 katika mkutano wa dharura wa kijiji cha Ihanga kilicholenga kujadili mambo mbali mbali likiwemo suala la sababu zilizopelekea kusimama kwa ujenzi wa choo cha wanafunzi katika shule ya msingi Ihanga.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Juma Ndelwa akisoma taarifa ya matumizi ya fedha shilingi milioni tano ambazo zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa choo cha wanafunzi shuleni hapo, amesema kiasi cha fedha kimetumika katika shughuli mbali mbali za shule nje a Choo ikiwemo kununua miche ya parachichi ya kupanda shuleni hapo.

kufuatia maelezo hayo wananchi wa kijiji cha Ihanga hawakupendezwa na maelezo hayo kwa kuwa mipango ya pesa hizo ilikuwa kujengea choo cha wanafunzi shuleni, hivyo kusababisha malumbano makali mkutanoni hapo.

Kutokana na kujitokeza kwa hali ya kukosekana utulivu kwa wananchi kutokuwa na imani na suala hilo diwani wa kata ya Ukwama Agustino Tweve ametoa siku 7 kuanzia leo kwa kumuagiza mwenyekiti wa kamati ya shule kukaa na kamati yake ili waweze kulifuatilia suala hilo na waje na majibu ya kina ya kuwaeleza wananchi
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Philipo Sanga amegoma kutekeleza maagizo ya Mh Diwani huku akidai hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi yake yuko tayari kuzipokea.

Mheshimiwa diwani Tweve baada ya kusikia kauli ya mwenyekiti wa kamamti ya shule Bw. Philipo Sanga kukaidi agizo lake amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa endapo ataona utekelezaji wa agizo hilo ambalo linalalamikiwa na wananchi halitafanikiwa.

Chanzo : GreenFm Tanzania 

Maoni