Makonda apiga STOP Mabaraza ya kata Dar.

 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesimamisha shughuli zote za mabaraza ya kata mkoani humo pamoja na kesi zote hadi hapo utaratibu wa kupitia upya taaluma za wanasheria waliopo katika mabaraza hayo utakapofanyika.

Makonda ametoa kauli hiyo leo Februari 10, 2018 katika ukumbi wa Diamond Jubilee katika mkutano wa kupokea taarifa za malalamiko ya wananchi yaliyowasilishwa kwa wanasheria wa mkoa huo.

Mkuu huyo wa mkoa amewataka makatibu wa tarafa wote kuanzia Februari 12, 2018 kuanza kutembelea mabaraza hayo.

Pia, amewataka wakurugenzi kuanzia Februari 12, 2018 kuanza kupitia wasifu wa wakuu wa idara na kazi zote wanazofanya na kuamuru wakuu wa idara ya ardhi katika Manispaa ya Ubungo na Ilala kupangiwa kazi nyingine.

Amesema wanapaswa kusimamishwa kwa sababu migogoro katika maeneo yao ni mingi kuliko wanayoitaja, jambo linaloonyesha kuwa hawako makini.

Katika mkutano huo, Makonda amesema malalamiko mengi ya wananchi hao yanaonyesha kuwa mhimili wa mahakama haufanyi kazi sawasawa.

Amesema mhimili huo ungefanya kazi yake vizuri, wananchi wasingekimbilia katika vyombo vingine badala ya mahakamani.

Amesema wananchi hawana imani na mahakama ndiyo maana wanapeleka kesi na malalamiko yao kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

Amefafanua kuwa wananchi wanashindwa kutofautisha mahakama na Serikali ndio maana wakikosa haki katika mhimili huo wanailalamikia Serikali na kutoa hukumu kwenye sanduku la kura.

“Wanailaumu Serikali ya CCM bure ilhali baadhi ya watendaji wa mhimili huo kukiuka wanachotakiwa kufanya, ”amesema Makonda.

Amesema kuna tofauti kati ya kuingilia mahakama na kuisaidia mahakama juu ya kutoa haki.

“Mahakama haitaki kuguswa kwa kisingizio cha mhimili mwingine, wamechukua nafasi ya Mungu na mimi ni mteule wa Mungu lazima niwaseme”amesema Makonda.

Amebainisha kuwa anaheshimu mahakama kama mhimili unaojitegemea lakini uvumilivu wake unafika mwisho kutokana na kutotoa haki.

“Nafahamu sheria zao ndio zinatoa hukumu, lakini mwisho wa siku haki inatolewa na Mungu” amesema.

Mwananchi

Maoni